Sunday, December 7, 2014

Kafulila

MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kusini David Kafulila, amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, ni kipimo halisi cha kuona kama Watanzania wameridhika na serikali ya CCM kutochukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa  akaunti ya Tegeta escrow.

Kafulila amesema hayo muda mfupi mara baada ya kuwasili mkoani Kigoma, ambapo amepata mapokezi makubwa kutoka kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, kama shujaa wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, na baadaye kusisitiza kauli hiyo alipohutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwanga Center, mjini Kigoma.

Amesema kukipigia kura Chama cha Mapinduzi CCM, katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa katika mazingira ambayo serikali yake imeshindwa kuchukua hatua katika ufisadi uliowekwa wazi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzo Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, ni kuonyesha kwamba wanaunga mkono ufisadi.

“nitoe wito kwa watanzania kwamba wanapaswa kuonesha hasira zao na uchaguzi huu wa serikali za mitaa ni kipimo kama watanzania tumekasirika ama hatujakasirika kutokana na ufisadi huu,”alisema Kafulila.


“uchaguzi huu ni kipimo kwamba haturidhishwi na jinsi mambo yanavyokwenda. Wanafunzi wamekosa mikopo kwa sababu serikali haina pesa, leo hii wananchi wanachangishwa fedha kwa ajili ya maabara wakati kuna watu wamepora zaidi bilioni 300!
Katika mazingira kama hayo wananchi wanapaswa kuonesha hasira zao, na moja ya njia za kistaarabu za kuonesha hasira ni kukataa kuchagua chama ambacho kinafanya maovu haya.”

Kauli hiyo ya Kafulila imekuja kufuatia baadhi ya vyombo vya habari kumnukuu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nauye, akisema kuwa CCM haina mpango wa kuchukua hatua zozote dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo.

Katika maelezo yake Nape alikaririwa akisema kuwa:

“Suala hili lipo chini ya Bunge na hivyo chama hakijaingilia kati na kuchukua hatua wabunge wake waliotajw. “Hatujawachukulia hatua (waliotajwa), wala hatuna mpango wa kuwachukulia hatua kwa sababu suala hili haliko ndani ya CCM… liko ndani ya bunge, labda kama litaingia ndani ya chama ndiyo tutalitolea maamuzi.”

Nape alikuwa akijibu swali kwamba suala la akaunti ya escrow litaathiri vipi chama chake kwenye uchaguzi kama rais Jakaya Kikwete atachelewa kuwawajibisha waliohusika na suala hilo kwa mujibu wa maazimio ya bunge ambapo Nape alijibu kuwa wao kama chama halitawaathiri chochote.

Kufuatia kauli hiyo David Kafulila amesema tafsiri ya kauli hiyo ni kwamba CCM inawatazama raia wa Tanzania kama watu ambao hawana ufahamu wa kutosha.


“unaposema kwamba hatutachukua hatua kwa watu ambao wanalalamikiwa na nchi nzima na kwamba hilo halituathiri kwenye uchaguzi, tafsiri yake ni kwamba pengine wana namna nyingine ya kushinda uchaguzi zaidi ya utaratibu wa kawaida ambao watu wanapigia kutokana na hisia zao, kutokana nay ale ambayo wanayaona,”aliongeza Kafulila.

Akisisitiza kauli yake Kafulila amesema nchi inapita katika kipindi kigumu ambacho kinahitaji mshikamano wa wanyonge kuweza kusimama kuhakikisha kwamba taifa linarudi kwenye mstari.


“tushikamane bila kujali itikadi za vyama tukijua kabisa kwamba tunachokifanya ndio njia pekee ya kuhakikisha taifa hili linabaki kuwa nchi moja; msipofanya hivyo nchi hii itasambaratika.”

Kauli ya Nape imekuja siku chache baada ya chama hicho kutoa msimamo wake dhidi ya wabunge wa chama hicho waliohusika katika sakata hilo kuwa bunge lichukue hatua stahiki. Nape, akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika ziara ya kukagua, kuhimiza na kusukuma utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/15 mkoani Mtwara, walisema kila aliyehusika katika kashfa hiyo, abebe msalaba wake.

Nape alisema chama hakiwezi kulea maovu yanayofanywa kinyume na kanuni na taratibu za chama hicho, hivyo kama bunge limebaini waliokiuka maadili wachukuliwe hatua stahiki dhidi yao. Kwa upande wake Kinana alisema muda wa kulindana na kubebana ndani ya chama umeisha na anayekiuka taratibu na kanuni za chama hicho awajibishwe na akishindikana achie ngazi.


 Msafara wa mapokezi ya Kafulila umefunga barabara ya Lumumba Mjini Kigoma.

 Msafara wa magari uliopmpokea Kafulila Airport Kigoma, ukimsindikiza hadi Hoteli ya Tanganyika Beach

POSTED BY WAVUTI

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!