Friday, February 6, 2015

SERIKALI imeingilia kati manyanyaso wanayopata wafanyabiashara ndogo na mamalishe nchini, kwa kuamua kuunda kikosi cha kiofisi, kitakachohusisha wajasiriamali hao kwa lengo la kukubaliana juu ya maeneo na muda mwafaka wa kuendesha shughuli zao. 



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliliambia Bunge jana kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imewasilisha mapendekezo hayo kwake, juu ya hatua za kutatua tatizo hilo.
 
Pinda alisisitiza kwamba wazo hilo la Tamisemi ni jema, na alitaka mkutano kwa ajili ya utekelezaji wake, uanze wiki ijayo ili waweze kuandaa utaratibu mapema iwezekanavyo.
 
Alisema hayo akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyesema baadhi ya wabunge wamekuwa wakihoji juu ya manyanyaso ya wafanyabiashara wadogo, mama lishe na waendesha pikipiki (bodaboda).
 
Alisema, lakini kwa kipindi chote Waziri Mkuu amekuwa akitoa maelekezo juu ya tatizo hilo, lakini mamlaka zinazohusika, haziko tayari kutii amri yake. “Je unawaambia nini Watanzania?” alisema Mangungu.
 
Akijibu, Pinda alisema matatizo yanayokumba wajasiriamali hao ni makubwa na si kwa Jiji la Dar es Salaam pekee, bali nchi nzima hivyo serikali imeamua kutafuta ufumbuzi wa kudumu na dhamira ipo.
 
“Jana (juzi) nimepata taarifa kutoka Tamisemi, wanaleta mapendekezo kwangu juu ya mapendekezo ya kutatua tatizo hilo. Katika taarifa yao, wamependekeza kwamba wataunda kikosi cha kiofisi kitakachofanya kazi kupitia makundi ya viongozi wa wamachinga nchini. Watakubaliana nao juu ya maeneo yatakayotumika na muda muafaka wa kufanya shughuli,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kikubwa alichoona katika mapendekezo ya Tamisemi, wametaka suala la usafi katika maeneo yatakayotumika kwa biashara, lipewe kipaumbele.
 
Alisema wataanza na Jiji la Dar es Salaam kufikia maelewano na vyombo vyote vinavyohusika, vitaeleweshwa juu ya maafikiano hayo kabla ya mkakati huo kusambaa kwenye majiji na miji mingine.
 
Alisema suala la kutenga maeneo kwa ajili ya biashara kwa siku maalumu, si la Tanzania pekee kwani liko kwenye nchi nyingi.
 
“Hata nchi za nje wana Sunday markets (masoko ya Jumapili). Hakuna tofauti na hili,” alisema Pinda na kusisitiza kwamba amekubaliana na Tamisemi jambo hilo walipe kipaumbele tofauti kuliko ilivyokuwa awali.
 
Kwa muda mrefu, katika miji mikubwa nchini kumekuwa na msuguano wa mara kwa mara baina ya mamlaka katika miji husika na wafanyabiashara, kiasi cha kuonekana kama mamlaka husika hufanya unyanyasaji wa makusudi dhidi ya wafanyabiashara hao.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!