Thursday, November 13, 2014


Wanakijiji wanaokaa karibu na shule hiyo wakishuhudia shule hiyo ikiwaka moto huku wakishindwa kutoa msaada wowote kutokana na gari la zimamoto la mkoa wa Pwani kushindwa kufika kwa madai kuwa ni bovu
Moto umezuka katika Shule ya Msingi ya Filbert Bayi, Kibaha, mkoani Pwani na kuteketeza majengo kadhaa yakiwamo mabweni mawili ya wanafunzi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. milioni 700.


Mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Bayi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 8:00 usiku wakati wanafunzi wakiwa wamelala na kuteketeza vyumba 14 vya madarasa, mabweni mawili ya wanafunzi na ofisi moja ya walimu. 


Alisema katika tukio hilo ambalo inawezekana chanzo chake ni kukatika katika kwa umeme shuleni hapo, wanafunzi 70 waliokuwa wamelala ndani ya mabweni hayo waliokolewa na walimu.

Bayi alisema vitu vilivyoteketea ni vitanda na magodoro na kwamba baada ya kutokea kwa tukio hilo, walipiga simu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kibaha ili wasaidie kuzima moto huo, lakini walifika eneo la tukio baada ya saa mbili na kukuta vitu vyote vimeteketea.

Bayi alisema hata walipopiga simu Kikosi cha Zimamoto Kibaha kuomba msaada, hawakuupata baada ya kujibiwa kuwa gari ni bovu na kuwalazimu kuomba msaada Zimamoto kutoka jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema moto huo uliteketeza mabweni mawili la wavulana na wasichana, madarasa 14, ofisi moja, maktaba, ukumbi wa chakula na darasa moja la kompyuta na kuwa uchunguzi unaendelea.



POSTED BY NIPASHE...

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!