Kumetokea shambulizi katika shule
moja ya upili wakati wanafunzi wakiwa wamekusanyika shuleni humo mjini
Potiskum Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Hata hivyo hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi kufikia sasa ingawa duru zinasema kuwa wanafunzi kadhaa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Shambulizi lilitokea wakati wanafunzi wakiwa wamekusanyika wakati wa asubuhi. Mji wa Potiskum ambapo shule hiyo ipo, umekuwa kitovu cha mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Boko Haram.
Shule hiyo ni ya mafunzo ya sayansi. Mwalimu mmoja alinukuliwa akisema kuwa alisikia mlio mkubwa wa kutisha wakati bomu hilo lilipolipuka.
Kundi la wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram huenda ndilo limefanya shambulizi hilo, ila taarifa bado hazijathibitisha hilo.
Kadhalika kundi hilo limekuwa likishambulia shule katika harakati zake za miaka 5 likitaka kuunda dola ya kiisilamu huku likipinga elimu ya kimagharibi.
Wiki jana shambulizi la kujitoa mhanga lilifanyika mjini humo na kuwaua watu 15 wakati wa maandamano ya kidini.
POSTED BY BBC
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment