Monday, November 10, 2014

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na daktari Bingwa Mpasuaji Edward Shaeffer muda mfupi kabla ya kuingia kwenye chumba cha upasuaji uliofanyika katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore Maryland Marekani Jumamosi asubuhi.Upasuaji huo uliochukua muda wa saa moja na nusu ulifanyika salama.


Habari kutoka hospitalini hapo zinasema Rais Kikwete anaendelea vyema na leo asubuhi alianza mazoezi ya kutembea, kuashiria kwamba mambo yote ni mswano. Tutaendelea kwuashirikisha taarifa ya maendeleo yake mara kwa mara. Tuzidi kumuombea apate nafuu haraka ili arejee nyumbani
kulijenga Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alfajiri ya jana, Jumamosi, Novemba 8, 2014, alifanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.


Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa Rais alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.

Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa. Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.

Wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.

Imetolewa na

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
DAR ES SALAAM,
NOVEMBA 9, 2014


 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Liberata Mulamula aliyekwenda kumjulia hali katika hospitali ya John Hopkins iliyopo Baltimore, Maryland, nchini Marekani, leo Jumapili, siku moja baada ya kufanyiwa upasuaji wa Tezi Dume.


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Dkt.Edward Shaeffer wa hospitali ya Johns Hopkins na Daktari wa Rais Profesa Mohamed Janabi(kulia) baada ya kuwasili katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore, Maryland, Marekani kwa upasuaji Jumamosi asubuhi. Upasuaji huo uliochukua muda wa saa moja na nusu ulifanyika salama.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!