Saturday, November 1, 2014


Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akisema suala la ruzuku na viti maalumu ni changamoto kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hicho si kipaumbele. 
 
“Tunachokitaka ni kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha tunaing’oa CCM madarakani kwanza, masuala mengine kuhusu ruzuku tutaweka utaratibu maalumu baadaye,” alisema.
 
Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana Jumatatu na Jumanne iliyopita.
 
“Wenzetu Kenya waliweza kuungana na kuhakikisha wanaking’oa chama tawala madarakani, lakini sasa kwa hapa mkiungana na kuwa chama kimoja ni lazima msajili chama chenu, sasa tunachokitaka ni kushirikiana tu kwanza,’’ alisema.
 
Alisema suala la ruzuku na uteuzi wa viti maalumu siyo lengo kuu la Ukawa inayoundwa na vyama vinne; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD kwa kuwa linajadilika. Alisema jambo la msingi hivi sasa ni ushirikiano wa amani.
 
Alisema kinachotakiwa kwa viongozi wa Ukawa ni kuaminiana kwanza ili kulinda muungano huo ambao alisema umeshaanza kukitikisa chama tawala, CCM.
 
Maazimio ya Baraza Kuu
Alisema Baraza hilo lilisisitiza umuhimu wa kuaminiana miongoni mwa vyama washirika katika ngazi zote ili kudumisha umoja huo na kufikia lengo la kuitoa CCM madarakani.
 
“Baraza limetaka uwepo utaratibu mzuri na wa wazi utakaoonyesha mambo ya msingi ambayo vyama vinavyounda Ukawa vimekubaliana. Utaratibu huu uwafikie viongozi wa ngazi zote za chama ili kuhakikisha jukwaa la Ukawa linatumika kwa lengo na dhamira iliyopo ndani ya hati ya makubaliano ambayo ni kuing’oa CCM madarakani,” alisema.
 
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa Profesa Lipumba alisema Baraza limetaka sheria irekebishwe ili uchaguzi wa diwani ufanyike pamoja na wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji kwa wakati mmoja, kwa vile diwani ndiye kiongozi mkuu wa kuchaguliwa wa kata.
 
Baraza hilo pia limetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utengenezwe utaratibu ambao utaifanya Tume hiyo kuwa huru kuwezesha chaguzi zote zijazo kufanyika kwa uhuru na haki.
 
“Taarifa za Tume zilieleza kuwa itaandikisha wapigakura mpaka kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji, kwa hiyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa usubiri mpaka daftari la kudumu la wapigakura likamilike na ndilo litumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema.


Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu la CUF, limesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha kupitishwa na kutangazwa kwa katiba hiyo na Bunge la Katiba lililoongozwa na Samuel Sitta akisema halikuzingatia sheria na taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
 
“Ni ukweli usiofichika kwamba mchakato mzima wa kupitisha katiba haukuwa na mwafaka wa kisiasa, kanuni za uendeshaji wa bunge hilo zilikiukwa na Katiba yote inayopendekezwa haikupigiwa kura ya mwisho,” alisema
 
Profesa Lipumba alisema, katika vikao vya ushauriano na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais Jakaya Kikwete alikubaliana na viongozi hao kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya, hususan kura ya maoni uahirishwe mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
 
“Mwanasheria wa Serikali alitangaza kura ya maoni Machi 30, Rais akiwa China alisema Aprili, yaani tayari tarehe imeshatangazwa kabla hata ya daftari la wapigakura kukamilishwa,” alisema.
 
Alisema baraza hilo pia limesikitishwa na utaratibu unaofanywa na NEC juu ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapigakura akisema hadi sasa hatua za uandikishaji hazipo wazi na wadau wengi hawana taarifa za kutosha juu ya nini kinaendelea.
 
Alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012, zinaonyesha kuwa kuna vijana zaidi ya milioni 4.6 ambao watafikisha umri wa kuwa wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 lakini bado hawajapewa fursa ya kuandikishwa huku wananchi wengi wakiwa wameshapoteza vitambulisho vya kupigia kura.
 
Alisema Juni, 19 mwaka huu, Nec, ilitangaza kufuta matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa na badala yake itatumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), ikiwa ni maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alinukuliwa akisema katika Kura ya Maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu, mpigakura atatumia kitambulisho kipya baada ya kuandikishwa upya katika mfumo huo na si vinginevyo.
 
Pia alisema Baraza Kuu linalaani vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na sheria vinavyoendelea kufanywa na Serikali kwa kulitumia Jeshi la Polisi.
 
Alitoa mfano wa masheikh waliokamatwa Zanzibar na kuhamishiwa Dar es Salaam na kufunguliwa kesi akisema walijitokeza mbele ya Mahakama na kusema waziwazi kwamba wamefanyiwa mateso na vitendo vya kinyama lakini hakuna hatua zilizochukuliwa ikiwamo kupelekwa hospitali.
 
Kadhalika, alisema baraza hilo limepokea kwa mshangao taarifa za utoaji wa uraia unaofanywa na Serikali kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi. Alisema uamuzi wa kuwapa uraia wakimbizi katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani ni mbinu ya kudhoofisha upinzani kwa kuwa wakimbizi wanaopewa uraia wanahamasishwa kuwa wachague chama tawala.
 
Kuhusu ardhi alisema: “Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi ya kutosha kwa raia wake, ugawaji wa mapande makubwa ya ardhi kwa wawekezaji yataleta mtafaruku wa uvunjifu wa amani na kuwafanya raia wazawa kuwa maskini wa kudumu,’’ alisema Profesa Lipumba.
 
Kuhusu maradhi hatari ya ebola, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limeitaka Serikali kuwa makini ili usiingie nchini akisema limesikitishwa na taarifa ya kwamba mpaka sasa nchi haina vifaa vya kuthibitisha kuwapo kwa vimelea vya ebola.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!