KATIKA hali isiyokuwa ya
kawaida, juzi kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu
wilayani Kahama mkoani Shinyanga, juzi kilisimama kwa muda baada ya
kutokea ugomvi wa kurushiana maneno na kejeli kwa baadhi yao, huku
wengine wakiomba kikao kisimamishwe angalau kwa dakika kumi ili
wapigane.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya Diwani wa Kata ya Idahina, Sospeter Bunanda (Chadema) kusimama na kutoa ushauri kwamba wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya Kata, wapewe semina ya uendeshaji wa mabaraza hayo kuliko kutumia vipeperushi walivyopewa na Mwanasheria wa halmashauri hiyo ili kuwajengea uwezo mkubwa wa kutatua migogoro ya ardhi katika kata zao.
Kufuatia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Sabasabini, Emmanuel Makashi (CCM) alisimama na kumwomba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Kimisha, kutupilia mbali maombi hayo. Alisema kusema hiyo ni kumfundisha mwanasheria, ambaye tayari ana taaluma yake.
Alisema alikasirishwa na tabia ya diwani huyo kuwa huwa anaingilia wachangiaji wengine wakati hajaruhusiwa na Mwenyekiti.
Bunanda alisimama tena na kuomba mwongozo kwa mwanasheria kwamba “Ni halali Serikali kuendesha vikao vyake kwa kutumia vipeperushi”? Ndipo vurugu ya maneno, ilitawala ndani ya ukumbi huo, ambapo Makashi alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri kumpatia dakika 10 ili ampige makonde Bunanda, akimtuhumu kwamba anapinga mabaraza hayo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba uniruhusu dakika kumi tu tupigane na huyu jamaa, na sitafungwa jela wala kesi yoyote, niruhusu Mwenyekiti maana anadakiadakia tu muda wa watu wengine kwa kuchangia hoja ambazo ni za kupinga, na asituletee Uchadema hapa,” alisema Makashi kwa jazba.
Kufuatia hali hiyo iliyodumu kwa takribani dakika tano, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Kulwa Shoto aliingilia kati na kukemea kitendo hicho. Aliwaomba madiwani hao, kutotumia kauli kali ambazo zinaweza kusababisha vurugu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kimisha aliwataka madiwani kutambua sheria, kanuni na miongozo ya Baraza la Madiwani pamoja na kuwa wavumilivu juu ya kauli na maoni ya wengine.
Hata hivyo, hali ilirejea kawaida na kikao hicho kuendelea kama kawaida, ambapo pamoja na mambo mengine Kimisha aliwataka madiwani kutumia muda wao kuhamasisha maendeleo katika kata zao, hususani kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete la ujenzi wa maabara tatu kila Shule ya Sekondari.
- HabariLeo: Diwani aomba dakika kumi apigane mkutanoni
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment