Tuesday, November 18, 2014

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia), akiwakabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe ripoti ya Uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu kashfa ya kuchota fedha zaidi ya sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow zilizohifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, imeanza kufanyiwa kazi na Bunge na ndani ya siku nane zijazo, umma utajua ukweli wake. Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikabidhi ripoti hiyo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, jana bungeni, na kamati imeanza kazi mara moja. Kwa mujibu wa Ndugai, taarifa hiyo ya CAG ina maoni kwa kila hadidu za rejea kama chombo hicho kilipoagiza wakati ilipotoa kazi kwa mkaguzi huyo.

Aliiagiza kamati hiyo ya Zitto iichambue zaidi na kutoa ushauri wake kwa Bunge kwa kuzingatia ushauri wa CAG pamoja na ushahidi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo iliwahoji wahusika wote wa sakata hilo.

Aliitaka kufanya kazi chini ya Kanuni za Nyongeza za Bunge pamoja na ile ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushughulikia suala hilo linalosubiriwa kwa hamu baada ya mjadala wa muda mrefu nchini.

Ndugai akimwakilisha Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimkabidhi Zitto mbele ya baadhi ya wajumbe wake ripoti hiyo pamoja na juzuu nne kubwa (viambatanisho) vya kuhusu ripoti ya sakata hilo.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikabidhi ripoti hiyo kwa Ofisi ya Spika wiki iliyopita, kabla ya jana Ndugai kuikabidhi kwa Kamati ya Zitto anayesaidiwa na Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa (CCM).

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Zitto alisema atazingatia maelekezo ya Spika ili kuhakikisha wanakamilisha kazi na mchakato mwingine wa kibunge uchukue nafasi yake. Aliwaambia wanahabari baadaye kuwa kamati hiyo katika kushughulikia ripoti hiyo, itafanya kazi zake kiuchunguzi, tofauti na inapofanya kazi nyingine.

Safari hii kamati itafanya kazi zake kiuchunguzi zaidi, haitakuwa kama mlivyozoea (waandishi wa habari), kuwa kamati iko wazi inapoendesha majukumu yake.

“Hii ni kutokana na ukweli kuwa isitoe mwanya kwa wanaotuhumiwa kuja kulalamika na kueleza kuwa Kamati ilikwisha kuwatia hatiani,” alifafanua Zitto.

Lakini aliwahakikishia wanahabari na Watanzania kuwa hakuna mtu yeyote atakayeachwa katika kushughulikia ripoti hiyo kwa kadri ilivyomhusisha.

Alisema kwa kuanzia, watamwita CAG na kisha wahusika wa Takukuru, kabla ya kuendelea na wahusika wengine waliotajwa.

Kwa upande wake, Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliwapongeza wanahabari kwa kufichua sakata hilo, akisema Bunge limefikia hapo kwa msaada wa waandishi wa habari.

Alisema siku nane kwao ni nyingi, kwani kazi hiyo ingeweza kufanyika kwa muda mfupi, hivyo wataikamilisha na kuwasilisha kwa wakati. Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea sasa hapa, ripoti hiyo imepangiwa kuwasilishwa bungeni Novemba 27, mwaka huu.

Naye Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alimkabidhi Zitto timu ya watendaji wake wa kufanya kazi na kamati hiyo kuanzia jana na itaendesha vikao vyake kwenye Jengo la Hazina mkoani hapa.

Mbali ya Dk Kashillilah, baadhi ya wajumbe wa PAC na maofisa wengine wa Bunge, makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.

Sakata la Tegeta Escrow linahusu uchotaji wa Dola za Marekani milioni 200, huku taarifa za awali zikidai kuwa CAG amebaini kuwa madai ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa IPTL ni Sh bilioni 321, wakati fedha zilizokuwa kwenye akaunti ni Sh bilioni 306.

Akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kibiashara kati ya Tanesco na IPTL, kampuni inayofua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar es Salaam.



 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akikabidhi Ripoti maalumu ya CAG Kuhusu akaunti ya ESCROW kwa Mwenyekiti wa PAC Mhe. Zitto Kabwe na Kaimu wake Mh. Deo Filikunjombe,Bungeni mjini Dodoma leo.

 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akikabidhi Ripoti maalumu ya CAG Kuhusu akaunti ya ESCROW kwa Mwenyekiti wa PAC,Mhe. Zitto Kabwe.

 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akiwa ameshikilia vitambu vilivyo Beba ripoti ya CAG kuhusu akaunti ya ESCROW Kabla ya kumkabidhi Mwenyekiti wa PAC Mhe.Zitto Kabwe leo.


0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!