Tuesday, November 18, 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman aliyemtembelea na kumjulia hali Jumapili Novemba 16, 2014 katika hoteli maalumu jirani na Hospitali ya Johns Hopkins jijini Baltimore, Maryland, Marekani anakoishi baada kutoka katika hospitali hiyo alikofanyiwa upasuaji wa tezi dume. Kushoto ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete. Jaji Mkuu yuko Marekani kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine yeye na ujumbe wake watahudhuria mkutano maalumu wa kimataifa wa Mabadiliko ya Sheria ya Ushahidi jijini Washington na pia kukutana na taasisi mbalimbali za fedha na marafiki wa maendeleo katika ili kupata wabia wa ujenzi wa maendeleo ya mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Novemba 16, 2014 alikutana na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mohammed Chande Othman na ujumbe wake.

Aidha, Rais Kikwete amewashukuru Watanzania kwa maelfu ya salamu za upendo kwake zikimtakia heri aweze kupona ambazo Rais amekuwa anapokea.

Rais Kikwete pia huenda akatolewa nyuzi katika siku tatu zijazo ikiwa maendeleo yake yataendelea kuwa ya kasi kama ambavyo imekuwa tokea alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume Novemba 8, mwaka huu, katika Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Maryland, Marekani.


Rais Kikwete alikutana na kuzungumza na Jaji Othman na ujumbe wake waliofika kumjulia hali katika Hoteli Maalumu ambako Rais Kikwete anaishi baada ya kutolewa Hospitali. Hoteli hiyo iliyoko Baltimore ina uhusiano wa karibu na Hospitali ya Johns Hopkins.

Mhe. Rais alimhakikishia Jaji Mkuu na ujumbe wake pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kwamba hali yake imeimarika na kwamba anachosubiri sasa ni kuondolewa nyuzi katika sehemu aliyofanyiwa upasuaji.

Alisema kuwa baada ya kuondolewa nyuzi ndipo madaktari wake watakapofanya tathmini ya mwisho kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani.

Jaji Mkuu amekuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa kumtembelea Rais Kikwete toka alipofanyiwa upasuaji Novemba 8, 2014.

Rais Kikwete alimwambia Jaji Mkuu kuwa sasa afya yake imeimarika zaidi, huku akiendelea kufanya mazoezi kiasi cha mara nne ama tano kwa siku.

Rais amewakumbusha Watanzania kuhusu umuhimu kwa watu kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuondoa shaka ya kupata tatizo kubwa kwa kuchelewa kugundua ugonjwa kwa wakati.

Alisema kwa upande wake yeye aliwahi kwenda kuchunguzwa na kwamba tatizo liligundulika mapema.

Kuhusu hali yake Mhe. Rais amesema kwamba masharti ya daktari ni kwamba nyuzi za upasuaji wa tezi dume aliofanyiwa huondolewa siku 12 baada ya kufanyiwa huo upasuaji, na kwamba Novemba 20, 2014 ndiyo siku ambayo amepangiwa kurudi hospitali kufanya hivyo.

“Baada ya kuondolewa nyuzi madaktari watanifanyia tathmini ya mwisho na endapo kama kutakuwa hakuna tatizo lolote nitaruhusiwa kurudi nyumbani”, alisema Dkt. Kikwete.

Jaji Mkuu na ujumbe wake wa watu wanne wako nchini Marekani kwa ziara ya kikazi ambapo watahudhuria mkutano wa kimataifa wa kujadili mabadiliko ya sheria ya ushahidi pamoja na kukutana na taasisi mbalimbali za fedha, ikiwa ni juhudi za mahakama hiyo kupata wabia wa uendelezaji wa ujenzi wa taasisi hiyo.

Wakati huo huo, Mhe Rais Kikwete amewashukuru wananchi kwa salamu za upendo za kumtakia nafuu wakati akiwa anaendelea na matitabu yake nchini Marekani.

Rais Kikwete, ambaye Jumatano, Novemba 12, 2014, alitoka wodini katika Hospitali ya Johns Hopkins na kuhamishiwa kwenye Hoteli Maalum jirani na hospitali hiyo, amesema ameguswa na kufarijika sana kwa maelfu ya salamu anazopokea kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kupitia namba maalumu ya kuwasiliana naye.

“Kwa kweli nimeguswa, nimefarijika na kutiwa moyo sana, sana kwa salamu za upendo za kunitakia heri nipate nafuu haraka pamoja na dua za wananchi kutoka kila kona ya nchi na kila pembe ya dunia”.

“Sina cha kuwalipa zaidi ya kusema tafadhalini pokeeni shukurani zangu nyingi sana kwa salamu hizo za upendo”
, alisema Rais Kikwete.

Pia ametoa shukurani nyingi kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi mbalimbali, ambao nao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa kumpa pole kwa njia mbalimbali.

Rais Kikwete amekuwa akipokea takriban ujumbe mfupi kiasi cha 1,200 kwa siku toka alipotoa namba yake maalum ya simu (+1-646-309-2295), ambapo wananchi wanawasiliana naye moja kwa moja kwa njia ya ujumbe mfupi ama SMS.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

17 Novemba, 2014




Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman aliyemtembelea na kumjulia hali Jumapili Novemba 16, 2014 katika hoteli maalumu jirani na Hospitali ya Johns Hopkins jijini Baltimore, Maryland, Marekani anakoishi baada kutoka katika hospitali hiyo alikofanyiwa upasuaji wa tezi dume.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman aliyemtembelea na kumjulia hali Jumapili Novemba 16, 2014
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe Ibrahim Juma ambaye ni mmoja wa wajumbe wa msafara wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman walipokwenda kumjulia hali jijini Baltimore, Maryland, Jumapili Novemba 16, 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na  Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Liberata Mulamula aliyesindikiza   msafara wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman walipokwenda kumjulia hali jijini Baltimore, Maryland, Jumapili Novemba 16, 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Ignass Kitusi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa msafara wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman walipokwenda kumjulia hali jijini Baltimore, Maryland, Jumapili Novemba 16, 2014


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mhe Hussein Katanga. ambaye ni mmoja wa wajumbe wa msafara wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman walipokwenda kumjulia hali jijini Baltimore, Maryland, Jumapili Novemba 16, 2014

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Meja Jenerali Adolph Mutta ambaye alimsindikiza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman kwenda kumjulia hali jijini Baltimore, Maryland, Jumapili Novemba 16, 2014

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman pamoja na ujumbe wake waliopomtembelea na kumjulia hali


0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!