BARAZA
la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), limesema kuwa halitaacha kuwaeleza
wananchi mapungufu yaliyopo kwenye Katiba Pendekezwa kwani Rais Jakaya
Kikwete ndiye aliyeanza kampeni kabla ya wakati ya kuhamasisha wananchi kuipigia kura ya ndiyo.
Aidha,
limesema likimaliza ziara hiyo ya kanda ya Ziwa Magharibi, watarudi
bungeni kuihoji serikali sh bilioni 2.5 zinazotarajiwa kutumiwa na Ikulu
kwenye vyombo vya habari kushawishi kura ya ndiyo zinatoka kwenye fungu
gani na zilipitishwa na bunge lipi.
Hayo
yalisemwa juzi na Mbunge wa Viti Maalum, Suzani Lyimo, wakati
akiwahutubia wananchi wa Tarime kwenye uwanja wa Serengeti akiwa
ameambatana na Makamu wa BAWACHA Taifa, Hawa Mwaifunga, Katibu Grace
Tendega, Naibu Katibu Kunti Yusuph, wabunge wa viti maalum Ester Matiko,
Grace Kiwelu na Chiku Abwao.
Alisema
kuwa, Rais Kikwete ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuanza kampeni ya
kuipigia chapuo katiba pendekezwa, kwani hata wakati akipokea mwenge wa
Uhuru aliwasisitiza wananchi kuipigia kura ya ndiyo kwa madai kuwa ni
nzuri.
“Labda
wachukue sindano na uzi watushone midomo yetu vinginevyo tutaendelea
kuwaeleza wananchi ubovu wa Katiba pendekezwa…Rais Kikwete akipokea
Mwenge wa Uhuru tulimsikia akifanya kampeni waziwazi, akiwaambia
wananchi kuwa katiba pendekezwa ni nzuri na ikifika wakati wa kuipigia
kura wasiache kuipa kura zote za ndiyo,” alisema Lyimo.
Alisema
kuwa, inashangaza kuona wakati Rais akidai kuwa muda wa kampeni kwa
ajili ya katiba bado, lakini viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), wameweka hadharani nyaraka zikionyesha kuwa Ikulu wanatenga sh
bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha kampeni ya kura za ndiyo kupitia
vyombo vya habari.
“Tukirudi
bungeni tutaenda kuhoji hizi sh bilioni 2.5 zinatoka kwenye fungu gani
na zinatolewa kwa utaratibu upi, wakati kwenye bajeti tuliyopitisha ya
mwaka 2014/2015 wa fedha suala hili halikuwepo,” alisema Lyimo huku
akishangiliwa na wananchi.
Tendega aendelea kulia michango ya maabara
Katibu
wa BAWACHA, Grace Tendega, alisema kuwa wataendelea kupinga wafanyakazi
wa umma kukatwa mishahara yao bila kuridhia kwa ajili ya kuchangia
ujenzi wa maabara mpaka serikali itakapofuata sheria.
Alisema
kuwa, hawapingani na ujenzi wa maabara lakini wanachokataa ni utaratibu
unaotumika kukusanya fedha za ujenzi huo ambao umegeuka kero kwa
watumishi wa umma na wananchi maskini wa vijijini, ambao wengine
huwalazimu kukimbia makazi yao kujificha kutokana na hali ngumu ya
uchumi inayowakabili.
“Narudia
tena kusema kama kweli Rais Kikwete ana nia ya dhati na mpango huu wa
ujenzi wa maabara kwenye shule za kata, basi apunguze bajeti yake ya sh
bilioni 50 aliyotengewa kwa safari za nje ya nchi, aipeleke ikatekeleze
ujenzi huo,” alisema Tendega.
Kunti ataka Polisi wanaoua wananchi Tarime wachukuliwe hatua
Naibu Katibu wa BAWACHA Taifa, Kunti, alisema kuwa inasikitisha kusikia
kuna wananchi wanaouawa na polisi huko Nyamongo maeneo ya kuzunguka
mgodi wa dhahabu wa North Mara, lakini hakuna hatua zozote za kisheria
zinazochukuliwa dhidi yao.
Alisema
kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo
inapotokea polisi wanaua raia ni lazima wachukuliwe hatua za kisheria,
kwani hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutoa uhai wa Mtanzania
na kikanyamaziwa, kwani nchi inaendeshwa kwa utawala wa sheria.
“Tunataka
wale wanaoua vijana wetu kule Nyamongo, wachukuliwe hatua za sheria
wafikishwe mahakamani kwa makosa ya mauaji, hatukubaliani na mauaji ya
aina hii kwenye Taifa huru na tunawaahidi wana Tarime tuko tayari
kuungana na nyie kuandamana mpaka mgodini kupinga mauaji haya wakati
wowote mkituhitaji,” alisema Kunti.
CHADEMA wampiga marufuku Makonda kukanyaga Mara
Katibu
wa CHADEMA mkoani Mara, Chacha Heche, amemtaka Kiongozi wa Chipukizi wa
UVCCM, Paul Makonda, kuwaomba radhi Watanzania kwa vitendo vya utovu wa
nidhamu alivyomfanyia Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba,
vinginevyo asikanyage mkoa huo.
Alisema
kuwa haiwezekani vijana wa Tanzania kunyamazia vurugu alizofanyiwa
kiongozi huyo Mstaafu aliyelitumikia Taifa kwa uadilifu kutokana na
misimamo yake ya kutetea maslahi ya umma kwenye rasimu ya katiba, hivyo
akasisitiza kuwa kama Makonda hataomba msamaha basi aishie eneo la
Rubana mpakani mwa mikoa ya Mwanza na Mara.
Matiko ahoji uprofesa wa JK aliopewa China
Mwenyekiti
wa BAWACHA mkoani Mara, Ester Matiko, alisema kuwa uprofesa aliopewa
Rais Kikwete nchini China, unaibua maswali mengi hasa ukizingatia tuhuma
nzito zilizoibuliwa hivi karibuni na vyombo vya habari vya kimataifa
vya BBC kuwa msafara wa rais wa China, Xi Jinping uliokuja nchini mwaka
jana uliondoka na pembe za ndovu.
Matiko
ambaye pia ni mbunge wa viti maalum, alisema kuwa utata wa uprofesa huo
unazidi kuibua maswali hasa ikizingatiwa kuwa wakati Rais huyo wa China
alipofika hapa nchini alisaini mikataba 28 ya gesi na mafuta ambayo
mpaka sasa ni siri, hata wao kama wawakilishi wa wananchi hawaijui.
Ziara
ya BAWACHA kanda ya Ziwa Magharibi mpaka sasa imetumia siku 21, ambako
wamefanya mikutano kwenye mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu na
Mara.
POSTED BY MARAYETU...
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment