Wednesday, November 12, 2014


Upasuaji huo inaarifiwa ulifanyiwa wanawake 83 kwa saa sita 

Kwa nini wanawake wa India wana mazoea ya kufunga kizazi?

Wanawake 11 nchini India wamefariki baada ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga vizazi vyao katika kambi ya matibabu hayo katika jimbo la Chhattisgarh.


Operesheni hizo zilifanyiwa wanawake 83 katika muda wa saa sita.
Maafisa wamekana madai ya ulegevu lakini maswali yanaulizwa ikiwa sera ya kudhibiti idadi ya watu nchini India ina mapungufu.

Inaarifiwa kuwa idadi ya watu huongezeka kila dakika nchini India.

Je watu India wana uraibu wa kupanga uzazi?'

 Wanawake wengi wanaokwenda kufanyiwa upasuaji wa kufunga kizazi hutoka katika jamii maskini 

India ni nchi ya pili duniani kwa wingi wa watu ikiwa na watu bilioni 1.27 na inatabiriwa kuwa nchi hiyo itaipiku China ifikapo mwaka 2030 kwa idadi ya watu.

Mnamo mwaka 1947, India ilijipatia uhuru, idadi ya watu wake ilifika milioni 345. Ina maana kuwa katika miaka 67 iliyopita idadi hiyo imeongezeka kwa watu milioni 900.

Ingawa kiwango cha kuzaana kimeshuka, ongezeko la wtau linasemekana kutokana na kiwango cha chini cha watu kufariki, kwani inoenekana wanaishi kwa miaka mingi sana.

Kutokana na wasiwasi wa idadi ya ongezeko la watu , maafisa wa utawala wanajaribu kuwashawishi watu nchini India kuwa na familia ndogo.

India ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuanzisha mpango wa kitaifa wa uzazi wa mpango miaka ya sabini ilipoanzisha kampeini ya kitaifa kuwahasi wanaume.

Zaidi ya wanaume milioni sita walihasiwa katika mwaka mmoja hadi pale kampeini hiyo ilipozua ghadhabu kitaifa.

Mtaalamu mmoja wa uzazi anasema kuwa watu nchini India wana mazoea ya kufanya mpango wa uzazi.

'Je wanaume na wanawake wanakabiliwa shinikizo sawa kufanya uzazi wa mpango?'

Baadhi ya wanawake waliofanyiwa upasuaji wanasema ilichukua dakika tano pekee 

Inakisiwa kuwa asilimia 37 ya wanawake walioolewa nchini India wamefungwa kizazi.

Kitendo cha kuhasi wanaume ni rahisi ikilinganishwa na operesheni za kuwafunga kizazi wanawake na ndio maana wanaume wengi wanafungwa kizazi kuliko wanawake.

Serikali mara kwa mara hufungua kambi ambako wanawake wanafanyiwa upasuaji wa kufunga kizazi bila malipo. Wanawake wengi sana huja katika kambi hizi hasa wanawake maskini.

Wanawake hawa huhaidiwa pesa ikiwa watakubali kufanyiwa upasuaji huo. Maafisa wa afya ambao huwashawishi wanawake kufanyiwa upasuaji huo pia hulipwa.
 
'Je sheria inasema nini?'

Serikali kwa mda mrefu imekuwa ikijaribu kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa mpango wa uzazi na umuhimu wa kuwa na familia ndogo.

Ikilinganishwa na China, India haina sera ya mtoto mmoja lakini imekuwa kwa mda mrefu ikitumia sera ya kuzawadi wanaokubali kupanga uzazi pamoja na kuwawekea vikwazo baadhi wanaopata watoto wengi.

Katika miaka mitatu iliyopita, serikali ya kitaifa pamoja na ile ya jimbo zimekuwa zikizawadi kwa pesa wafanyakazi wa umma wanaochagua kufunga kizazi.

'Nini hatari ya operesheni za kufunga uzazi?'

 Maafisa wa afya wamekana madai ya kuwa walegevu kazini kama chanzo cha wanawake 11 kufariki 

Sio mara ya kwanza kwa operesheni kama hizi kwenda mrama.

Mnamo mwaka 2012, wanaume watatu walikamatwa kwa kuwafanyia upasuaji wanawake 53 bila ya kutumia dawa za kuzuia uchungu.

Ingawa maafisa wakuu nchini humo wanasema upasuaji huo haufanyiwi mtu kwa lazima wanaharakati wanasema mpango huo huwalazimisha wanawake kufanyiwa upasuaji.

Wanawake wengi hulazimishwa na waume zao kufanyiwa upasuaji ili wapate kuzawadiwa na serikali.

Wanawake wengi wanaokuja kufanyiwa upasuaji huu hutoka kwa familia masikini.

POSTED BY BBC
 

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!