Wednesday, November 12, 2014


WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), 54 akiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Pemba wilayani Tarime Mkoa wa Mara, Augustino Wantora, wamejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA).
Wanachama hao wa CCM walipokelewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), Hawa Mwaifunga, kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Kutehuguma Kata ya Pemba.

 
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Wantora alisema kuwa wameamua kuhama CCM baada ya chama hicho tawala kukumbatia wala rushwa na kuwanyanyasa wale wanaoipinga.
"Nikiwa CCM nilikataa rushwa nikajenga maadui wengi, yaani wale wote nilioziba mianya yao ya rushwa wakaamua kunishugulikia kwa hila na uongo, sasa mimi na wenzangu tumeamua kuja CHADEMA…
"Tumekuja huku kwa sababu tunajua ni chama kinachopigania haki za wanyonge, tutafanya kazi na wale wanaopenda kula fedha za wananchi tutaendelea kuwadhibiti," alisema mwenyekiti huyo.
Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanateua viongozi wenye sifa kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Alisema kuwa wahakikishe wanajua vema mipaka ya vijiji na vitongoji vyao kabla ya kujiandikisha au kujaza fomu za kugombea, ili kuepuka kuzuiwa kugombea au kupiga kura.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA mkoani Mara, Chacha Heche, aliwataka wampe taarifa pindi watakaposumbuliwa na polisi na viongozi wa serikali kwa kutundika bendera za CHADEMA kwenye nyumba zao.
"Mkikamatwa na polisi kwa kosa la kujiunga na CHADEMA au kupepea bendera mnipe taarifa mara moja nikakutane na hao polisi, kwa sababu CHADEMA ni chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria," alisema Heche.
Naye Naibu Katibu BAWACHA Taifa, Kunti Yusuph, aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanahamasisha, wanajitokeza kupiga kura na kuzilinda.
Alisema kuwa mabadiliko wanayoyataka watayapata kijijini hapo endapo watajitokeza kwa wingi kumpigia kura kiongozi anayefaa ambaye anapatikana CHADEMA
POSTED BY MARAYETU

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!