Thursday, June 19, 2014


WATU zaidi ya 30 wanashikiliwa na polisi wilayani Muleba katika Mkoa wa Kagera, wakituhumiwa kufanya vurugu na uharibifu wa mali, chanzo kikiwa kifo cha mfanyakazi wa ndani aliyefia mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, George Mayunga alisema vurugu hizo zilitokea baada ya mwili wa mtoto huyo, Asera Tryphone (16) kufikishwa katika Kijiji cha Bukono kilichoko Kata ya Muleba.

Kwa mujibu wa kamanda, binti huyo alikuwa akifanya kazi za ndani mkoani Arusha, akaugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Mount Meru kabla ya kukutwa na mauti, Juni 12 mwaka huu. Mwajiri wake, Valentina Maxmilian, alisafirisha mwili huo na baada ya kuufikisha kijijini hapo, inadaiwa wazazi wa marehemu walikuwa wamepata taarifa tofauti kwamba mtoto wao alifariki dunia kutokana na kipigo na mateso.
Aidha, taarifa zilizokuwa zimeenea kijijini hapo ni kwamba, baadhi ya viungo vya mwili, hususani sehemu za siri, mkono na mguu, vilikuwa vimekatwa jambo lililohusishwa na ushirikina. Kamanda alisema wazazi walitaka mwili huo ufanyiwe uchunguzi kabla ya kuupokea.
Waliamua kupiga simu Kituo cha Polisi cha Muleba, na Polisi ilitaka kuongozana na ndugu hao hadi Kituo cha Afya cha Kaigara kwa ajili ya uchunguzi. Hata hivyo wanafamilia waligoma na kutaka polisi wafanye uchunguzi wa mwili huo nyumbani jambo ambalo halikuafikiwa. Baada ya polisi kuondoka eneo hilo, inadaiwa wanafamilia walimbeba maiti na kumtelekeza katika barabara iliyoko karibu na Kituo cha Polisi Muleba.
Polisi walichukua mwili na kuupeleka Kituo cha Afya cha Kaigara. Polisi walishauri ndugu hao kusubiri mganga aliyekuwa zamu aufanyie mwili uchunguzi wa kitaalamu jambo ambalo waliafiki. Wakati wakisubiri uchunguzi, wananchi walihamasishana tena na kuvunja mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti ambapo polisi waliamua kutumia nguvu na kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao.
Kulingana na maelezo ya Kamanda, baada ya kutuliza ghasia, uchunguzi wa mwili ulifanyika na ndugu wakaridhika na kwenda kuzika ingawa inadaiwa wapo baadhi ya watu waliokuwa wakishawishi wazazi wa marehemu wasikubali.
Inadaiwa usiku wa kuamkia jana, wananchi walijikusanya na kwenda Kijiji cha Buyango kilicho jirani na nyumbani kwa marehemu, na kuamua kuchoma nyumba mbili za Veronica Maximilian (mama wa Valentina, aliyekuwa mwajiri); ambaye anadaiwa ndiye alikwenda kuomba mtoto huyo kwa familia ya Tryphone Joseph (54) aende kufanya kazi Arusha. Kutokana na matukio hayo, polisi inashikilia watu hao wapatao 30 wakihojiwa kutokana na tuhuma za kuvunja mlango wa chumba cha maiti, kuchoma nyumba, kuhamasisha vurugu na kutelekeza mwili wa marehemu barabarani.
Miongoni mwa wanaoendelea kuhojiwa, yumo Veronica; anayedaiwa kumwomba mtoto huyo akafanye kazi kwa mwanawe. Pia Polisi imesema inaendelea kufanya uchunguzi wa kina mkoani Arusha alikofia mtoto huyo na pia kuchunguza nyumbani kwao. Wazazi wazungumza Mama mzazi wa mtoto huyo, Georgina Tryphone alisema aliombwa mtoto wake kwenda kufanya kazi za ndani Januari mwaka jana.
Alisema alikuwa akipata mawasiliano ya simu kutoka kwa mwajiri wake. Georgina alisema tangu Juni 12 mwaka huu, amekuwa, akipokea simu kupitia kwa mwajiri wake akielezwa kwamba binti yake atakwenda karibuni kuwasalimia.
Hata hivyo alidai, Juni 13 mwaka huu, alipigiwa simu na mwajiri huyo akimweleza kwamba mwanawe anaumwa. Alidai baada ya saa takribani mbili, alitaarifiwa amefariki dunia. “Mimi na mume wangu tulianza kujawa na wasiwasi juu ya mwanetu na hapo hapo tukapokea jeneza la maiti, lakini tulipotaka kufungua tukazuiwa na aliyeuleta akidai umeharibika,” alisema mama huyo.
Aliendelea kudai, “tulipokuwa tunalazimisha kuuona mwili tuliambiwa ugonjwa uliosababisha kifo chake unaambukiza hivyo ungeweza kuathiri wananchi waliokuwa katika familia yetu.” Taarifa hiyo ya mzazi inadai mwili huo ulikuwa na makovu na pia meno manne ya juu hayakuwepo. Mkuu wa Wilaya Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo, alisema katika kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alikutwa na viungo vilivyodaiwa kutokuwepo.
Isipokuwa alisema, kilicholeta utata ni kukutwa meno manne hayapo na mwili kuwa na makovu mbalimbali. Mkuu wa Wilaya amekemea wananchi kuendekeza imani za ushirikina na kusambaza taarifa za uongo zilizosababisha uvunjifu wa amani. Kwa upande wa familia ya mwajiri wa mtoto huyo iliyoko Kijiji cha Buyango pamoja na mwajiri husika, haikupatikana kuzungumzia madai hayo kutokana na hali tete iliyokuwa imewakabili.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!