Mfanyakazi wa ndani, Yusta Lucas (20) amekumbana na masahibu yanayofanana na yale ya mtoto Nasra Mvungi (4) aliyekuwa amefungiwa kwenye boksi kwa miaka karibu minne huko Morogoro. Huyu amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam akiuguza majeraha yanayotokana na kuteswa na kufungiwa ndani kwa miaka mitatu.
Binti huyo, mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, katika
Kijiji cha Kampala amedai kuwa amekuwa akiteswa na kufungiwa ndani ya
nyumba na tajiri yake, Amina Maige wa Mwananyamala, Kwa Manjunju katika
kipindi chote hicho.
Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha
Oysterbay kwa tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.
Akisimulia masahibu yaliyompata akiwa katika Wodi
Namba Tatu ya hospitali hiyo, Yusta alisema: “Nililetwa Dar es Salaam
mwaka 2010 kufanya kazi za nyumbani baada ya bosi wangu (Amina) ambaye
ni binamu yangu kuzungumza na mama yangu na kuniomba nije kumsaidia kazi
ndogondogo.”
Alisema aliishi vizuri na mwajiri wake huyo,
lakini mwaka 2012 ndipo mambo yalipoanza kubadilika akidai kuwa Amina
alianza kumwadhibu kwa kumng’ata na kumchoma kwa pasi kila alipomtuhumu
kutokufanya kazi zake vizuri.
“Alikuwa akinichapa na kuning’ata sehemu
mbalimbali wakati mwingine usoni, pia kunichoma kwa pasi yenye moto kila
aliponituhumu kutokufagia au kupiga deki vizuri.”
Hakuwahi kupelekwa hospitali
Alisema licha ya kupata vidonda kutokana na adhabu
hizo, mwajiri wake huyo hakuwahi kumpeleka hospitali na pale alipoona
hali ni mbaya alimnunulia dawa... “Tunaishi wawili tu baada ya kuondoka
mumewe na mtoto wake kumpeleka shule ya bweni... niliugulia hadi
nikapona bila mtu mwingine kufahamu.”
“Akienda kazini anafunga geti na kunikataza
kufungua hata kama mtu atagonga… sokoni nilikuwa naenda siku ambazo yeye
yupo tu na huwa akiniamrisha niende haraka na kurudi pasipo kuzungumza
na mtu yeyote.”
Alisema mwajiri wake huyo alikuwa akituma pesa za
mshahara wake kwa mama yake akisema ndiye anayepaswa kulipwa, jambo
ambalo anadhani limemfanya mama yake kuhisi mwanaye yuko katika mikono
salama... “Kila alipotuma alipiga simu na kunipa niongee na mama
kuhakikisha kama zimefika huku akinisimamia na baada ya hapo anachukua
simu.”
Ataka kurudi kwao
Binti huyo ambaye sehemu kubwa ya mwili wake ina
alama za kung’atwa meno na majeraha ya kuchomwa na pasi, alisema:
“Ninaomba mtu yeyote mwenye hela, nataka nikitoka hapa hospitali nirudi
Tabora kwa mama. Nina shaka na maisha yangu hapa kwa huyu mama… sitaki
tena kubaki Dar es Salaam kutokana na mateso ninayoyapata."
Polisi wasema
Mkaguzi Msaidizi wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Prisca Komba alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada ya majirani
kupeleka taarifa hizo katika Kikundi cha Kipange kilichopo Kwa Manjunju
ambacho nacho kilitoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa mwanamke
huyo ukawekwa.
Majirani walichukua hatua hiyo kutokana na kusikia
kelele za kilio mara kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
“Tumekagua makovu na majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na
kupata jumla kuwa yako 91,” alisema Komba na kuongeza:
“Toka jana amekuwa akinitaka nisiondoke mbali naye
amekuwa na hofu, lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri
na kumhakikishia kwamba hapa yuko salama.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Thobias
Edoyeka alisema suala hilo linashughulikiwa na polisi pamoja na ustawi
wa jamii, kauli iliyoungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa
Mwananyamala, Rose Temu ambaye alisema wanafuatilia kwa karibu matibabu
yake pamoja na usalama wake. “Hali yake ikishaimarika na kujiridhisha
kuwa anaendelea vizuri, tutakuwa na jukumu la kumuunganisha na familia
yake,” alisema.
Ofisa Muuguzi Msaidizi Wodi Namba Tatu ambayo ni ya kinamama, Rose Mussa alisema Yusta anaendelea vizuri.
“Anaendelea vizuri kwa kweli, jana (juzi) hakuwa
hivi alikuwa mwoga hawezi kujieleza tofauti na leo (jana)… bado
anaendelea na vipimo, tutakapoona anafaa kuruhusiwa tutafanya hivyo na
kumkabidhi kwa ustawi wa jamii.”
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment