Thursday, January 15, 2015

Shirika la Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) limezima mtambo wa Ruvu Juu kwa siku mbili, kutokana na kuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu, ikihitaji kubadilishwa, jambo litakalosababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma ya maji.

Ofisa Uhusiano wa Shirika hilo, Eva Lialo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia ubadilishaji wa vifaa hivyo katika mtambo huo na kuongeza kuwa marekebisho yalianza kufanyika tangu jana na leo.


Alisema matengenezo hayo yamekuwa ya haraka na dharura huku wakibadilisha vifaa vingine, ambavyo vilikuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu.


Alisema pia katika marekebisho hayo, watabadilisha nguzo zinazoshikilia mita ambazo zimelala sana na kuhatarisha usalama katika eneo husika.

"Kutokana na hali hiyo Shirika litafanya matengenezo hayo kwa haraka kwa siku mbili ambayo italazimu kuzima kabisa mtambo huo kwa siku mbili kwa masaa saba hadi 10,” alisema Eva.

Alisema kutokana na matengenezo hayo maeneo yafuatayo yatakosa maji kwa wakati huo ambayo ni maeneo ya Kimara, Mbezi, Makuburi, External, Mlandizi, Mburahati, Msewe, Changanyikeni na hata Kibamba.

  • HabariLeo.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!