MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha Mhe. Joshua Nassari
alikamatwa na kushikiliwa na jeshi la polisi kwa kutuhumiwa na tukio la
kumteka mtendaji wa kata ya Makiba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema Nassari alikamatwa majira ya saa moja usiku wa Desemba 16 katika eneo la Doli lililopo katika kijiji cha UsaRiver kwenye gari aina ya Land cruiser lenye namba za usajili T 753 AQR.
Alisema Nassari anatuhumiwa kumteka Mtendaji Kata aliyefahamika kwa jina la Nemani Ndundu wa Kata ya Makiba tarafa ya Mbuguni wilayani Arumeru mkoani Arusha Desemba 15 majira ya saa mbili asubuhi katika eneo la Maji ya Chai.
Mtendaji huyo alikumbwa na hayo alipokuwa katika pikipiki yake akielekea kwenye Kata ambapo ndipo inatuhumiwa kuwa Mhe. Nassari alimkamata na kumpiga na kumjeruhi katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku akimtaka amuonyeshe majina ya wanachama waliopiga kura katika kituo cha huduma na maendeleo kilichopo katika Kata yake .
Mhe. Nassari alifikishwa mahakamani katika wilaya ya Arumeru leo Desemba 17, 2014 kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hakimu David Mwita wa Mahakama ya mwanzo ya Maji ya Chai mkoani Arusha aliahirisha kesi dhidi ya Nassari hadi Desemba 24, 2014.
Madai ya tuhuma katika hiyo ni ya kuharibu mali ya umma yenye thamani
ya shilingi laki mbili, kumteka mtu na kumtishia kwa bunduki.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imemuachia Mbunge huyo baada ya kutimiza masharti ya dhamana, ikiwa ni pamoja na kuwa na wadhamini watatu ambao wana mali zisizohamishika zenye thamani ya shilingi milioni moja na nusu kila mmoja.
Akiongea mara baada ya kuahirishwa kesi hiyo, wakili wa Mbunge huyo, Bw. James Ole Milya alisema amesikitishwa sana na tukio la mahakama hiyo kumpa masharti makubwa mteja wake kwani kesi yake ilikuwa haihitaji mashariti makubwa hivyo.
Aidha, alisema kuwa angependa kesi hiyo ipelekwe katika mahakama ya Wilaya ili yeye kama Wakili wa Mbunge aweze kumtetea kwa kuwa Mahakama ya Mwanzo hairuhusu kuweka Wakili.



0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment