Friday, November 14, 2014

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo, kutoa adhabu kali kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Madimba na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mayanga, kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa maabara.


Pia ameagiza watendaji hao kushushwa vyeo kutoka Ofisa Mtendaji wa Kata hadi Mtendaji wa Kijiji, ambapo kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Mayanga, kwa sasa anatakiwa kuwa mwalimu wa kawaida.

Aidha, ametoa angalizo kwa watendaji wote wa halmashauri hiyo watakaoshindwa kuendana na kasi ya utekelezaji wa agizo la ujenzi wa maabara, kuwa ni bora watafute kazi zingine mapema.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya ujenzi wa maabara ndani ya wilaya yake.

Alisema kutotimiza majukumu kwa baadhi ya watendaji, ndiyo chanzo cha kudorora kwa ujenzi huo.
Alisema amelazimika kuchukua maamuzi hayo magumu kwa wakati huu wa utekelezaji wa maagizo ya kiongozi wa nchi, ili kutoa fundisho kwa watendaji wengine, ambao ni wazembe na wasioendana na kasi ya ujenzi wa maabara.

“Unajua unaweza kuwa mwalimu mzuri, lakini usiwe kiongozi bora mwenye uwezo wa kuongoza wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye eneo lako. Hivyo kwa mwalimu kama huyu pamoja na mtendaji wa kata, hawastahili kuachiwa waendelee kuzorotesha kasi ya ujenzi wa hizi maabara,” alisema. 

Akizungumza kwa njia ya simu, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Madimba, Mahamudu Mtota, alisema hajapokea taarifa za kupunguzwa madaraka na kwamba anachojua ni maagizo aliyoyatoa mkuu huyo wa wilaya alipokuwa Msimbati kuwa kesho (leo) asubuhi aende ofisini kwake.

Alisema ni kweli kuwa ujenzi wa maabara katika shule mbili za sekondari zilizoko kwenye kata hiyo unaenda kwa kusuasua, kutokana na kukosekana kwa vifaa vya ujenzi, ikiwemo mawe,mchanga pamoja na maji na kwamba hadi sasa maabara zote mbili ziko kwenye hatua ya msingi.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!