Friday, November 7, 2014

WAVURUMISHAO makombora dhidi ya Jaji Joseph Warioba wamekuwa wakitoa hoja kwamba mzee huyo muda wake wakuzungumzia suala la katiba mpya ulishamalizika kwa minajili kuwa Tume yake ya kukusanya maoni ya Katiba mpya ilishavunjwa.

Kelele zimepigwa katika bunge maalum la katiba, mtaani wanasema “mzee pumzika muda wako umekwisha” hawataki tena atumie uhuru wake wa kikatiba kuzungumzia mambo ambayo yeye anaona hayajaenda sawa, wao wazungumze yeye anyamaze, au sasa hivi kuna sheria inasema ni wakati wa Chama fulani tu peke yake kujimwaya mwaya uwanjani na kuipamba katiba pendekezwa.

Nafurahi wanaomkosoa Mzee Warioba wamekuwa wakijinadi kuwa wao ni wafuasi wazuri sana wa hayati Mwalim Julius Nyerere, wamekuwa wakitusihi kila uchao tuige yale mazuri aliolifanyia taifa hili, wanatwambia tutunze amani, tuache ubaguzi na mbwembwe za kila aina.

Wanatwambia Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele kulipigania taifa hili, alikuwa mzalendo, aliyapigania mataifa mengine ya Afrika, mfano wa Afrika Kusini, Msumbiji nakadhalika, kuhakikisha yanapata uhuru wao, hata Rais Kikwete kuhutubia mazishi ya Mandela na akaeleweka vema ni kutokana na jithada za Mwalimu alizozifanya huko nyuma katika taifa hilo.

Wakati wakimuona Mwalimu Nyerere kama mzalendo huku wakitutaka tumuige mzee huyo, kwa bahati mbaya wale wanaitika wito wao wakututaka tufanye hivyo wanawaona kama nuksi sasa, wanawatwisha majina ya kila aina, wavunja amani, wazushi, ni shidaaa na mengineyo.

Inawezekana Mzee Warioba anafahamu au hafahamu anayoyafanya sasa ndio alioyafanya Mwalim Nyerere ambae tunaambiwa alikuwa mzalendo wa dhati, alietayari kuifia nchi yake enzi za uhai wake, alipigania uhai wa mataifa mengine ya Afrika.

Kama kweli ndani ya mioyo yetu tunasukmwa na dhamira ya dhati ya kuwataka watanzania wamuenzi Nyerere kwa vitendo, basi Mzee Warioba anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Sote tunakumbukumbu nzuri tu, Mwalimu Nyerere aling’atuka madarakani baada ya kuwa Rais Wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hapo mwaka 1985, ndani ya miaka yake 14 yaani kabla ya kifo chake hapo mwaka 1999 akiwa amestaafu, hadi anaingia kaburini Nyerere hakuacha kuisemea Tanzania pale ambapo aliona mambo yanaenda mrama.

Baada ya Azimio la Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1990 chini ya utawala wa Rais mstaafu mzee Ally Hassani Mwinyi mashuhuri kama mzee Rukhsa, ambalo linaaminika ndio lilileta kifo cha azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere hakukaa kimya, roho ilimuuma kweli kweli akalalamika kila kona ya nchi kuwa Azimio hilo lilikuwa na kasoro gani hadi walitupe, mpaka sasa athari za kuuawa moja kwa moja kwa azimio hilo tunaziona.

Mwalimu Nyerere alilalamikia tabia za watu kadhaa ndani ya Serikali kujilimbikizia mali, alikuwa akilalamika mno suala la viongozi wa nchi hii kutumia rushwa ilia wapate uongozi, alisema “Kiongozi anaetaka kwenda ikulu kwa kutoa rushwa aogopwe kama ukoma.
Suala la kukubali na kutenda kila tunachoambiwa na benki ya dunia(WB) shirika la fedha la kimataifa(IMF) na nchi za magharibi Mwalimu alilipigia kelele sana, wapo walimuona kama hamnazo, athari zake tunaziona sasa, kwenye sekta ya elimu, afya, kilimo nakadhalika.
Leo tumekuwa taifa la ombaomba, dhana ya kujitegemea imetoweka kabisa vichwani, tupo hewani kama popo tukienda kulialia huku na kule tukitafuta wakutuamulia mustakabali wa taifa hili, kauli za siku hizi ni kuwa “Mradi huu tumejenga kwa ufadhili wa EU, n.k” ni nadra kusikia mradi huu tumeujenga kwa pesa zetu wenyewe, wazungu wanasema ‘He who pays the piper call the tune’ maana yake, anaegharamia kitu ndio chake. Hili lipo sasa wanatuamulia kila jambo nasi ni ndio mzee.Tusubiri kucheza ngoma ya ushoga.

Kwa kuzingata dhana ya kujitegemea na kutumia akili ya mbayuwayu kama alivyokuwa akitaka Nyerere, leo hii nchi ndogo ya Cuba yenye idadi ya watu takribani Milioni 10, nchi iliowekewa vikwazo na Marekani kwa miongo kadhaa, kwa kuzingatia dhana hiyo, imepeleka madaktari wapatao 165 kusaidia juhudi za kupambana na janga la Ebola huko katika nchi za Afrika magharibi zilizoathirika mno na ugonjwa huo.

Kwa kuwa si lengo langu kuijadili Cuba kuonesha namna gani imefanya jitihada kubwa zaidi ya ‘Uncle Sam’ na wafuasi wake katika kupambana na janga la Ebola, soma taarifa kamili katika anuani hii, commondreams.org/views/2014/11/02/moment-world-embraces-cuba-model-and-slaps-empire.

Mifano ipo mingi mno ya kuonesha namna gani Mwalimu Nyerere aliendelea kulipigania taifa hili kwa juhudi zake zote kuhakikisha linakuwa na muelekeo stahiki, licha ya kwamba alikuwa ameshastaafu ngazi ya Urais alioitumikia kwa takribani miaka 24.

Lakini wakati wote huo Mwalimu Nyerere alitoa mawazo yake alioamini ndio sahihi katika kuiendesha nchi, hakuna alieibuka na kusema “Mzee kaa kimya muda wako umeisha”, mwalimu aliachwa aseme atakavyo hakushambuliwa hata kidogo kama tunavyoona sasa.
Nasi kwamba watawala walikuwa wakifurahia jambo hilo, walichofanya ni kutumia busara na kumuacha atumie haki yake ya kikatiba, mwalimu alitoa hoja zake na wao wakatoa za kwao, hakukuwa na matusi na kashfa za hapa na pale.

Mwalimu alipolalamikia kuuawa kwa Azimio la Arusha, Mzee Rukhsa akamjibu kwa hoja kuwa “kila zama na kitabu chake” huku akitoa ufafanuzi kuonesha namna gani kifo cha Azimio la Mwalimu kilikuwa kimewadia kulingana na wakati husika, na hivyo kitabu kipya ni lazima, si Mzee Rukhsa wala wapambe wake waliomwabia nyerere anyamaze.

Wapo walioitwa wadhaifu, wengine wakaambiwa wamesilimu kisa wameomba msaada uarabuni, wakatungiwa vitabu, G55 wakakiona cha moto, wakachambuliwa na mwalimu Nyerere ila wakamuacha tu na kauli zake, hawakuunda kikundi cha wahuni kumshambulia. Nyerere akaachwa atambe, wao wakamchora tu.

Ukiifuatilia kwa makini hotuba yake yakulivunja bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania hapo mwaka 1995, utagundua Rais mstaafu Mwinyi alitumia hotuba hiyo iliochukuwa muda mrefu kujibu hoja nyingi za mwalimu Nyerere, alitoa takwimu na mifano ya kila aina kuuonesha umma kuwa wakosoaji wa serikali yake walikuwa wanamuonea tu kwani na yeye kafanya mengi sana tangu aingie madarakani hapo mwaka 1985.

Hadi Rais Mkapa anaingia madarakani mwalimu aliendelea kukosoa vikali yale ambayo aliamini si afya kwa taifa, kwa utamaduni wa wakati ule na kuwapa heshima viongozi waliolitumikia taifa hili huko nyuma kwa moyo wakizalendo tena CCM haijazaliwa ikiwa bado TANU, si Mzee Mkapa binafsi wala wapambe wake waliomwambia Nyerere akae kimya, walimuacha ‘apayuke’.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa viongozi wa wakati huo waliojawa na busara na kuheshimu wale wenye mawazo tofauti na yao, hususani waliowatangulia katika madaraka, waliwaheshimu hata kama hawakuyapenda yaliokuwa yakisemwa dhidi yao, kwani yapo waliyatii na mengine kuyapuuzilia mbali.

Mzee Warioba ana historia yake katika taifa hili,anaheshima zake,amelitumikaia taifa hili ipasavyo, hata wanaomshambulia yeye ni baba yao na wengine wajukuu, kwa bahati mbaya, hata walio ngazi za juu wameshindwa kuwakemea hawa vijana wa siku hizi kumsema vibaya mzee huyo, kibaya zaidi wameenda mbali hadi kutaka kumdhuru, taifa linawayawaya!

Warioba kama raia wa kawaida nae anatoa maoni yake kwa yale anayoyaona hayafai, hayakwenda sawa katika raismu ya katiba alioisimamia, hakatazi watu wasiisome katiba pendekekezwa bali anatoa elimu kama CCM wanavyofanya. Tuache fikra zipambane.

Yaliotokea Ubungo Plaza si kwa bahati mbaya, watanzania ninaowajuwa mimi hawajawa na ujasiri wa kiasi kile bila kuwepo nguvu fulani kubwa nyuma yao, hata hivyo kwenye siasa hakuna jambo linalotokea kwa bahati (coincidentally) mambo mengi hupangwa.Tusubiri tutaona mengi msimu huu.

POSTED BY WAVUTI

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!