Wahudumu wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa wamebeba masanduku ya kura za wajumbe waliopiga kura za siri kwa Sura ya 11 hadi 19 ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, mjini Dodoma jana.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliopiga kura za hapana wamelazimika kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar kwa madai ya vitisho walivyopata kutoka kwa wenzao.
Mmoja wa wajumbe hao, Salma Said alisema jana jioni kuwa yeye na wajumbe wenzake wamekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kwenye Kamati ya Mashauriano ili kuhojiwa kuhusu kura hiyo na kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa wajumbe wenzao wameamua kuondoka Dodoma.
Vitisho hivyo vimeripotiwa muda mfupi baada ya Sitta kuunda Kamati ya Mashauriano ya watu tisa inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan kushughulikia kura hizo zilizopigwa na wajumbe saba zinazoweka njiapanda uwezekano wa kupatikana akidi ya kupitisha Katiba inayopendekezwa.
Wajumbe waliopiga kura za wazi za hapana kwa ibara zote ni Adil Mohamed Adil, Dk Alley Soud Nassor, Fatma Mohamed Hassan, Jamila Ameir Saleh, Salma Hamoud Said, Mwanaidi Othman Twahir na Ali Omary Juma.
Kwa upande wa Tanzania Bara aliyepiga kura ya hapana kwa rasimu nzima ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi na wajumbe 30 kutoka Zanzibar wakipiga kura ya siri.
“Baada ya kupiga kura za hapana leo (jana), walijitokeza wajumbe akiwamo (jina tunalihifadhi kwa sasa) wakaanza kutuzongazonga,” alisema Salma.
“Walituambia kuwa tumebaki hadi dakika ya mwisho halafu tunasema hapana kwa rasimu nzima ili kula fedha za bure, wanasema bora tungeondoka na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Hata hivyo, alipopigiwa simu yake ya mkononi mmoja wa watuhimiwa, alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata simu na alipopigiwa mara ya pili alijibu alisema; “Mimi ni mheshimiwa mwana na niko Sudan.”
Salma alisema miongoni mwa wajumbe hao wakiwamo baadhi ya mawaziri waliwafuata hadi nje ya ukumbi wakiwatishia kuwa watawafanyia hujuma kwa kukataa kuunga mkono rasimu hiyo.
“Sisi tumeamua kuondoka kurudi kwetu, hatutaingia tena bungeni maana hivi vitisho vimezidi sasa,” alisema Salma.
Juhudi za kuwapata wajumbe wenzake kuzungumzia vitisho hivyo hazikuzaa matunda, lakini Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba amelichukulia kama suala la kisiasa.
Alisema wajumbe hao hawajasema wametishiwa kufanyiwa kitu gani, bali walimweleza kuwa wameambiwa kuwa wamekaa pale (bungeni) kwa ajili ya kupata pesa.
Kuhusu kukataa kwao kuhudhuria katika Kamati ya Mashauriano, Hamad alisema hawezi kulitolea jibu kwa kuwa litafanya maridhiano yasifanyike.
Kamati ya Maridhiano
Akitangaza kuunda kamati hiyo, Sitta alisema ana suala mbele yake ambalo linahitaji mashauriano chini ya Kanuni ya 54(4) kutokana na baadhi ya wajumbe kupiga kura ya hapana kwa ibara zote.
Kanuni hiyo inasema: “Mwenyekiti baada ya kushauriana na kamati ya uongozi anaweza kuunda kamati ya mashauriano pale linapojitokeza suala linalohitaji mashauriano.
“Baadhi ya wajumbe jana (juzi), walipiga kura za hapana kwa ibara zote, jambo ambalo haliwezekani kuwa hivyo. Kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti, nimeunda kamati hii ambayo naomba ikafanye kazi leo,” alisema.
Alisema kamati hiyo yenye wajumbe tisa itakayoongozwa na Samia na baada ya kikao chake cha jana itatoa matokeo bungeni. Wajumbe wengine ni Rashid Mtuta, Shamsi Vuai Nahodha, Omary Yusuf Mzee, Mohamed Aboud, Andrew Chenge, Dk Asha-Rose Migiro, Dk Francis Michael na Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi.
“Hawa watakaa na wale wawili walioniomba kwamba wanataka kusikilizwa kwa nini wamesema hapana kwa kitendo ambacho inaonekana kama wamepoteza muda kukaa bungeni ili kukataa Katiba yote,” alisema.
Alitoa nafasi kwa wajumbe wengine ambao walipiga kura za hapana watakaopenda kwenda katika kamati hiyo kueleza ni kwa nini waliikataa rasimu hiyo.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa upigaji kura jana, Sitta alisema kuwa hali inakwenda vizuri... “Inshallah hali inakwenda vizuri na dua la kuku halimpati mwewe.”
Kwa mujibu wa Kanuni 36(3). Endapo mjumbe baada ya kukataa ibara za Rasimu ya Katiba, mwenyekiti ataunda kamati ya mashauriano ambayo itasikiliza hoja zake na kupata mwafaka.
Kanuni 36 (4), baada ya kamati ya mashauriano kukutana na kujadili ibara inayobishaniwa, itapeleka taarifa ya matokeo ya mashauriano yake kwenye Bunge Maalumu kwa ajili ya kujadiliwa na ibara hiyo kama ilivyo au baada ya kuandikwa upya kwa kuzingatia taarifa ya Kamati ya Mashauriano.
Endapo theluthi mbili haitapatikana kwa mara ya pili, ibara hiyo itahesabiwa kuwa haikukubaliwa wala kupitishwa na Bunge Maalumu kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na kanuni hizi.
TEC yamshukia Sitta
Kauli ya Sitta kuwa baadhi ya nyaraka kuhusu mchakato wa Katiba Mpya zinazotolewa na makanisani, “hazina utukufu wa Mungu na ni za kipuuzi” imepondwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), likisema hajui nguvu ya umma.
Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alisema: “Unadhani tulivyotoa waraka tulikuwa tunawataka waumini wafanye nini? Je, ni kufuata dhehebu lako limesema nini au kufuata kilichomo katika waraka? Wewe (mwandishi) si Mkristo? Jibu hilo.”
Aliongeza, “Wenye mapenzi na nchi hii wamfute kichwani Sitta na huo upuuzi aliosema ni wake mwenyewe. Huyu anadhani kuwa ana akili kuliko mamilioni ya Watanzania waliopendekeza wanataka kujitawala namna gani?”
Sitta alitoa kauli hiyo mjini Dodoma juzi wakati akiwatambulisha viongozi 13 kutoka Jumuiya ya Image ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba ya mjini Dodoma.
Licha ya Sitta kutotaja taasisi husika, lakini Jukwaa la Wakristo Tanzania ndilo lililotoa waraka unaotaka kusitishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya na kusambazwa makanisani.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na TEC, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
“Anadhani wanaweza kutunga Katiba ya kuwatawala wananchi. Kauli aliyoitoa ni sawa na kuwapuuza Watanzania na ni sababu ya madaraka tu, maana ndiyo yanayowapa watu wengi kiburi,” alisema.
Askofu huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa kauli hiyo ya Sitta maana yake ni kwamba CCM itabaki milele madarakani na Watanzania hawawezi kuwafanya jambo lolote.
“Unajua mtu mwenye kiburi na dharau anayedhani hawezi kuambiwa chochote unatakiwa kumwacha kama alivyo ila Watanzania ndiyo watakaoamua nini wanataka katika maisha yao,” alisema.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Antony Lusekelo alisema: “Bunge la Katiba limemwelemea Sitta na ndiyo maana ameanza kutukana watu.”
Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako alisema kwa jinsi jamii ilivyogawanyika katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, ilikuwa jambo la busara kwa makanisa kutaka kusitishwa kwa mchakato huo mpaka makundi yote yanayovutana yafikie mwafaka.

chanzo: mwananchi
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment