Wednesday, August 6, 2014

Kamishna Kova akiwa na RPC mpya wa Temeke, Kihenya Kihenya

Jeshi la Polisi linamshikilia Inspekta wake, Celestine Makene (40) kwa madai ya kumpiga hadi kumsababishia kifo mtoto wa kaka yake, Alerd Makene (16). 
 
Makene anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 24, mwaka huu katika makazi ya polisi, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam na anashikiliwa katika Kituo cha Chang’ombe.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema marehemu Alerd alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mbagala Kuu.
 
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kifo chake unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa endapo itathibitika kuwa alitenda kosa hilo.
 
“Tunamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye pia ni askari polisi katika Chuo cha Polisi Kurasini, tutahakikisha kuwa haki inatendeka bila kujali nafasi aliyonayo mtuhumiwa,” alisema kamanda huyo.
 
Imedaiwa kuwa Makene alimwadhibu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mzazi wa jirani akimlalamikia kwamba Alerd alimpiga mwanaye hivyo kumtaka amkanye juu ya tabia hiyo.
 
Akizungumzia tukio hilo, jirani ambaye hakutaka jina lake kutajwa , alisema watoto hao walikuwa wakicheza mpira lakini kwa bahati mbaya Alerd alimpiga rafiki yake huyo usoni kwa mpira na baada ya kupigwa kwa mpira, alikwenda kwao kumshtaki.
 
“Usiku huo baba yake alimfungia chumbani na kumpiga kwa fimbo, ngumi na mateke kiasi kilichomfanya mtoto huyo kupiga kelele sana,” alisema na kuongeza kwamba majirani walijaribu kwenda kumwamulia lakini hakusikiliza.
 
Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa alisafiri kikazi Nairobi lakini akadai kuwa kabla ya kuondoka, aliamuru mtoto huyo asifunguliwe mlango.
 
Alidai kuwa baada ya mtoto huyo kulalamika sana, mama yake mdogo alimfungulia mlango na kumkuta akiwa amevimba uso na akivuja damu nyingi.
 
Alisema waliamua kumpeleka Hospitali ya Temeke kwa matibabu na alifariki dunia usiku wa Ijumaa Agosti Mosi.
 
“Baba yake alirudi haraka kutoka Nairobi alipopigiwa simu kuwa Alerd ana hali mbaya na alifahamishwa baada ya muda mfupi kuwa amefariki,” alisema.


Baba huyo aliporudi, alikwenda hospitali na kukuta tayari Alerd ameshafariki na polisi walimkamata baada ya kupata taarifa kuwa amefika hospitalini hapo.
 
Alipoulizwa kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mtoto huyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Amani Malima alisema polisi ndiyo wenye mamlaka ya kutoa ripoti hiyo kwa vyombo vya habari na kuwa wao walimaliza kazi yao na kuwakabidhi.
 
Hata hivyo, Kihenya alisema polisi wanayatumia matokeo ya uchunguzi wa daktari katika kukamilisha uchunguzi wao na baada ya kukamilika atatoa taarifa kamili kuhusu kifo hicho.
 
Hadi jana, utaratibu wa kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Musoma kwa maziko ulikuwa ukifanyika.
Posted by Mwananchi...

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!