Wednesday, August 6, 2014

Wanamgambo wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria, ambao chanzo chake kinatajwa kuwa ni ukosefu wa ajira na ujinga.



Rais mstaafu wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo (aliyeinama) akimuonyesha kitu Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, katika mkutano wa marais wastaafu uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
SIRI ya kuanza kwa kundi la ugaidi la Boko Haram linaloendesha vitendo vyake vya kigaidi nchini Nigeria, iliyofichuliwa wiki iliyopita na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Olusegun Obasanjo, sasa inaweza kuiathiri Tanzania.
Obasanjo, akiwa katika kikao na viongozi wenzake wastaafu jijini Dar es Salaam, alisema ukosefu wa elimu na ajira kwa vijana wa nchi hiyo ndiyo chimbuko la Boko Haram.
Onyo hilo la Obasanjo kwa serikali za Afrika kujikita katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira na elimu linaweza kuwa chachu kwa viongozi wa Tanzania kutafuta ufumbuzi badala ya kushambulia wanasiasa.
Obasanjo aliongeza kuwa kundi la Boko Haram ambalo linatokea kusini mwa Nigeria, limekusanya wapiganaji wengi ambao hawana ajira, huku wengi wao wakiwa hawajapata elimu na ajira.
Akitoa ushauri kwa nchi za Afrika kuondoa tatizo hilo ili kuhakikisha uchumi wake unakua na kuondoa uwepo wa makundi kama hayo yanayosababisha kushusha uchumi, ni lazima wahakikishe wanatoa elimu na kutengeneza ajira kwa vijana wa mataifa yao.
Wito kama huo umewahi pia kutolewa na viongozi kadhaa nchini, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, waliotaka kutafutwa kwa ufumbuzi wa tatizo la vijana wasiokuwa na ajira.
Lowassa, amekuwa akielezea namna ambavyo ukosefu wa ajira unavyotengeneza bomu kwa vijana linalosubiri kulipuka muda wowote, akitolea mfano wa kujitokeza kwa vijana 10,000 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakiwania nafasi 70 pekee za kazi Idara ya Uhamiaji.
Katika mazungumzo yake, Lowassa aliwaeleza wanahabari kwamba ili kuepusha ongezeko hilo linalokua kwa kasi, serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Lowassa aliyejiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amekuwa akiishauri serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira, ambalo limemsababishia malumbano na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka aliyejibu mapigo Machi 21, 2012 bungeni kwa kutoa takwimu zinazoonyesha namna serikali ilivyotengeneza ajira.
Kwa upande wake, Mbowe alilalamikia serikali kwa kutokuwa makini kwa kushindwa kulitafutia ufumbuzi tatizo la ajira kwa vijana ambalo aliomba liwe hoja maalum bungeni, serikali kuu, halmashauri na katika baraza la mawaziri kwani ni janga la taifa.
Wakati Mbowe akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha bungeni kuhusu mapendekezo ya serikali ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15, alisema ajira ni mkakati na siyo suala la kufumania.
Akielezea njia za kuondoa tatizo hilo, aliishauri serikali kubadili mfumo uliopo wa kurundika kila kitu serikali kuu katika kutengeneza ajira kwani haiwezi kufanikiwa na badala yake alitaka kuwe na mkakati wa kutengeneza ajira katika halmashauri zote 133.
Mbowe alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na wakurugenzi na wataalam wa uchumi katika halmashauri wasiokuwa na uwezo wa kutengeneza ajira.
Aliishauri serikali kuanzisha Mamlaka ya Majengo (Real Estate Authority – REA) itakayohusika kusimamia majengo mijini na kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia kujenga ajira kwani bila ya kufanya hivyo, vijana watalazimika kukimbilia mijini kwa sababu vijijini hakuna maendeleo wala mwelekeo.
Alisema ni aibu kwa halmashauri za Kinondoni na Ilala kutegemea ruzuku toka serikali kuu wakati zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kusaidia kutengeneza fedha na ajira kwa vijana.
Aliongeza kuwa idadi ya Watanzania kwa sasa wanafikia milioni 50 na kila mwaka wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya 40,000 huku kukiwa hakuna ajira.
Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa kutovalia njuga kupuuza ushauri huo kunaweza kuchangia kushamiri kwa makundi ya kihalifu kama Boko Haram aliyoitaja Obasanjo.
Tayari hapa nchini kumezuka makundi ya kihalifu ambayo baadhi yao ni Watoto wa Mbwa, Panya Road na Badface ambayo yalitikisa maeneo mbalimbali kwa uhalifu uliozimwa na vyombo vya dola, lakini unaweza kuzuka tena siku za usoni.
Vijana hawa wamekuwa wakienda kupora wakiwa kundi kubwa lenye watu 30 hadi 100 wakiwa wamebeba silaha za jadi ambazo huzitumia kuwashambulia wanaowapora.
Zipo taarifa nyingine zinasema kwamba vijana hao hutumia njia ya kuimba kwa sauti kubwa wimbo huu; “Tunatakaa… pesa zetuu..!” huku wakiingia ndani kuchukua vitu vya thamani na kuwaacha baadhi ya majirani wakiduwaa kwa kudhani mtu anadaiwa kumbe anaibiwa.
Makundi ya vijana hawa yanaelezwa kuwa maskani yao yapo maeneo ya Manzese, Kigogo, Mburahati, Kigogo Luhanga na viunga vyake.
Vijana wanaofanya uhalifu kama huo, pia wamekuwa wakipatikana katika Mkoa wa Mara wakitumia majina ya Jamaica Mob, Mbio za Vijiti na Midomo ya Furu ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwasumbua wakazi wa mkoa huo kwa kuwaibia na baadaye kuwajeruhi kwa silaha za jadi.
Mkoani Kilimanjaro pia liliibuka kundi la vijana lililokuwa likifanya uhalifu lijulikanalo kwa jina la Kunguru Hafugiki.
Tanzania Daima Jumapili, limekuwa likifuatilia baadhi ya nyendo za viongozi wa serikali katika kutatua kero za ajira, ambao wengi wao wamekuwa wakitoa zawadi za fedha na ahadi kwa vijana wakati wa uchaguzi badala ya kujikita kwenye miradi itakayokuwa endelevu.
Ahadi hizo na fedha hizo ndizo zinadaiwa kuwajenga chuki vijana pindi zinaposhindwa kutekelezwa na kujikuta wakishiriki kwenye vitendo vya kihalifu.
Posted by Tanzania Daima...

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!