Wednesday, May 28, 2014

MSHTUKO! Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Jeshi la Polisi mkoani hapa Morogoro, limelazimika kuwaita wafanyakazi wa chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kushuhudia mwili wa mtu aliyekutwa amekufa kwenye kichaka jirani na ofisi za makao makuu ya jeshi hilo.



Kwa mujibu wa polisi, mwili wa mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Juma Mbega (46) ulikutwa kwenye kichaka ukiwa umeharibika vibaya na kutoa harufu kali huku ukizungukwa na wadudu, nusura polisi wenyewe watoke nduki.

 
Akizungumza na paparazi, Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Afande Suzy alisema wakiwa ofisini, walisikia harufu kali hivyo kulazimika kufanya uchunguzi ndani na nje ya jengo hilo la polisi lenye ghorofa moja ambapo chini zipo ofisi za Jeshi la Polisi Wilaya ya Morogoro Mjini na juu za mkoa.

 “Baada ya kuchunguza harufu hiyo, tulibaini uwepo wa maiti kwenye kichaka kilichopo nje ya ofisi zetu ambapo mwili huo unaokadiriwa kuwepo hapo kwa zaidi ya wiki moja ulikuwa umeharibika vibaya na kutoa harufu kali,” alisema afisa huyo.
Kwa upande wake, Nuru Adam ambaye ni mjomba wa marehemu huyo, akizungumza na gazeti hili eneo hilo la tukio alisema: “Huyu ni mjomba’ngu, amezaliwa tumbo moja na mama yangu mzazi, Kilegu Hamis.

“Alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka hivyo huenda alikutwa na matatizo hayo akiwa eneo hili peke yake.”
Baada ya uchunguzi wa awali na ndugu wa marehemu kujulikana, maiti ilichukuliwa na kupelekwa mochwari kuhifadhiwa huku taratibu za mazishi kwa ndugu zikiendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Leonard Paul alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.


0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!