Viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na
Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa alitaka kuiba
ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi wakati Bunge
lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye uchotwaji wa
fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi
za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa kinyume na taratibu
za kibenki.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza Mwananchi kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza Mwananchi kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali tuhuma hizo
akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba kama
angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano
iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi chini ya
hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu ikisomwa
bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo la mbali
na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa nataka
kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya
maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale ya
awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye alikuwa makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa
walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo.
“Waziri Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Waziri Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa kuamkia Jumatano
ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo ndiyo ilikuwa
sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC kuwasilisha
taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana, Filikunjombe aligusia
suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa kushikamana katika
kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe alisema
walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kuilinda ripoti
yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo
kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa zilizokuwa na
nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza. Polisi ilidai
baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya
ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa
yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake, Bunge
lilimtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa kuhusika
kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu kutoka
kwenye akaunti hiyo.
Bunge pia lilitaka hatua za kisheria zishughulikie watu wote
waliohusika kwenye sakata hilo, wakiwemo wanasiasa waliopokea fedha za
mgao, taasisi za kifedha zilizohusika kufanikisha miamala haramu na
wafanyabiashara waliohusika.
Vikwazo
Akizungumzia vikwazo walivyokumbana navyo wakati
wa kutekeleza majukumu yake, Filikunjombe alisema kamati hiyo, iliyokuwa
na wajumbe 24, watatu wakiwa waalikwa, kati yao 19 kutoka CCM na watano
kutoka upinzani, walipata vikwazo vingi ikiwa ni pamoja na jaribio la
kurubuniwa.
Filikunjombe alisema wajumbe wa PAC waliamua kuwa
kitu kimoja na kuweka itikadi zao pembeni licha ya watu mbalimbali
kutumia fedha kutaka kuwagawa ili wasisimamie ukweli. “Unajua sakata la
Escrow linawagusa watu wenye fedha ambao walianza kuuaminisha umma kuwa
wajumbe wa PAC na sisi tumekula fedha hizo. CCM ilitakiwa kuuchukulia
wizi huu kama ajenda yake kuu,” alisema.
Alisema hakupendezwa na ushauri uliotolewa na
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kuhusu adhabu
wanazotakiwa kupewa watuhumiwa wa wizi wa fedha hizo, wakati na yeye
akiwa miongoni mwa watuhumiwa kutokana na kudaiwa kupewa Sh1.6 bilioni.
Kuhusu suala la watuhumiwa kujiuzulu, Filikunjombe
alisema siku zote Serikali haipendi kusimamiwa na Bunge, bali inapenda
kushauriwa na kwamba hiyo ndiyo sababu ya Serikali kukataa pendekezo la
PAC la wahusika kujiuzulu bila kuziomba mamlaka za uteuzi kutekeleza
hilo.
“Ukitizama suala la (mkataba wa ufuaji umeme)
Richmond si kama fedha zilichotwa wazi, lakini hili la escrow fedha
zimechotwa na waliochota wanajulikana, sasa iweje tushikwe na kigugumizi
kutaka wajiuzulu. Tena fedha hizo ni mara tatu ya zile za Richmond,”
alisema.
Zitto ataja vitisho
Kwa upande wake Zitto alisema: “Vitisho vilikuwa
vingi, lakini siyo kutoka serikalini bali kutoka kwa watu binafsi ambao
wanahusika na uchotwaji huu wa fedha.
“Mfano kupigiwa simu kuambiwa niachane na jambo
hili ama sivyo nitakufa au hata kutishiwa kuchafuliwa. Vipeperushi vya
matusi dhidi yangu vilisambazwa kwenye nyumba za wabunge ili kuniondolea
heshima na uhalali wa kuongoza vikao.”
Akieleza sababu za kuilinda ripoti, Zitto alisema:
“Kwa sababu Serikali ilikuwa inataka kuipata mapema ili kuichakachua,
hatukulala siku hiyo mpaka taarifa yetu ilipokuwa taarifa rasmi ya
Bunge. Mimi, Deo na Luhaga ndio tuliopewa jukumu hilo.”
Alisema hawakupata usumbufu kutoka serikalini, isipokuwa pale zilipoanza kujengwa hoja kuwa mahakama imezuia mjadala.
Alipoulizwa kama watuhumiwa wa sakata hilo waliwahi kumfuata kwa
namna yoyote ile alisema: “(Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen)
Masele peke yake ndiye alikuwa akiomba msaada. Maswi alinipigia simu
siku moja tu kuomba msaada, lakini sikumjibu kitu. PAC tunaamini kuwa
tumetenda haki kwa wananchi.”
Maswi alipopigiwa simu jana alipokea na mwandishi
alipojitambulisha, alikata simu na alipopigiwa tena kwa simu tofauti
alipokea na alipoulizwa swali hilo aliikata tena simu.
Ripoti ya PAC ilisomwa na kujadiliwa bungeni na kusababisha mtikisiko mkubwa kutokana na mapendekezo yake kuwagusa watu wazito ndani ya Serikali.
Ripoti ya PAC ilisomwa na kujadiliwa bungeni na kusababisha mtikisiko mkubwa kutokana na mapendekezo yake kuwagusa watu wazito ndani ya Serikali.
Watu wengine waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni
wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na
kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge.,
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria
na Utawala) na Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti).
Mapendekezo hayo yanataka Mwambalaswa, Ngeleja na
Chenge wavuliwe nyadhifa zao, sambamba na wote waliohusika katika
muamala wa Akaunti ya Escrow kuchukuliwa hatua baada ya uchunguzi.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment