KASHFA ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow, imewachafua viongozi watatu ambao walishaanza harakati za
kuusaka urais kwa mwaka 2015.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Kwa upande wa Pinda, ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) iliyowasilishwa bungeni, ilionyesha kiongozi huyo wa shughuli za
Serikali bungeni alilidanganya Bunge kwa matamshi yake.
Mara kadhaa Pinda alisikika akiueleza umma kuwa fedha hizo hazikuwa za umma bali mali ya Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya IPTL.
Katika maazimio ya PAC, Pinda alitakiwa pia kuwajibika kutokana na
kushindwa kusimamia Serikali kwani katika hatua zote za kutolewa kwa
fedha hizo, alikuwa akijulishwa.
Pinda ambaye alitangaza kuanza harakati za urais kimya kimya, akiwa
jijini London, Uingereza alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha BBC,
alijikuta kwenye wakati mgumu pale Bunge lilipopitisha azimio la
kumpeleka kwa mamlaka ya uteuzi kabla baadae jina lake kuondolewa.
Hali hiyo ilijitokeza pale Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
alipolishauri Bunge kupeleka majina ya watu wote waliotakiwa kuchukuliwa
hatua kwa mamlaka zao za uteuzi ili hatua zaidi zichukuliwe.
Baada ya kauli hiyo ya Zitto, Spika wa Bunge Anne Makinda alilihoji
Bunge na kwa sauti moja likakubali kabla ya Mbunge wa Simanjiro, Ole
Sendeka kusimama na kuomba mwongozo wa Spika ambaye baadaye alitengua
uamuzi wake.
Akizungumza na Mtanzania, Zitto alisema jina la Pinda kupelekwa kwa
rais ingetosha kuonyesha Bunge halina imani naye, hivyo mamlaka yake
hiyo ya uteuzi ingebidi itengue nafasi ya kiongozi huyo wa shughuli za
Serikali bungeni.
Alisema pia kamati yake ilikubali kuondoa jina la Pinda kwenye orodha
ya vigogo waliopaswa kushughulikiwa baada ya mazungumzo kati ya wabunge
wa upinzani na wale wa CCM.
Kutokana na hali hiyo, Pinda ambaye anajulikana zaidi kama ‘mtoto wa
mkulima’, harakati zake za kwenda Ikulu zimetiwa doa kwani mwanzo
alihesabika kuwa ni kati ya wagombea wasio na kashfa.
Kwa upande wake, Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, anadaiwa kupewa Sh milioni 40.4 kutoka kwenye akaunti ya Escrow
huku Profesa Tibaijuka ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, akidaiwa kupewa Sh bilioni 1.6.
Viongozi wote hao wawili ambao hawajawahi kutangaza rasmi kuwania
urais mbali na majina yao kutajwa kwenye orodha hiyo, Bunge limeazimia
wachukuliwe hatua.
Kwa upande wa Profesa Tibaijuka, rais ametakiwa kumvua wadhifa wa
uwaziri huku Ngeleja ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala, spika akishauriwa kumchukulia hatua ya kumvua
wadhifa huo.
Akichangia bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na
Uratibu, Steven Wasira, aliwataka wote wanaotumia suala la ripoti ya PAC
kwa vigezo vya kuwaondoa wenzao katika mbio za urais hawastahili kupewa
nafasi hiyo.
“Wanaotaka urais kama wapo ni pamoja na mimi, ambao wanaona mbinu ni
kuwaondoa wengine kwa nguvu, hao hawafai kupewa urais wa nchi hii. Urais
ni lazima ushindaniwe kwa haki na vyama vyote vipewe nafasi ya
kushiriki. Kama unataka urais ushindani uwe kwa njia sahihi,” alisema.
Alisema ni bora kuwa maskini anayeheshimika kuliko kukubali kuwa
tajiri anayedharauliwa na kutukanwa kutokana na mapato yasiyokuwa
halali.
Wasira alieleza kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) imesema baadhi ya watu walikwenda kuchukua fedha wakiwa na
magunia, mifuko ya sandarusi, rumbesa na maboksi katika moja ya benki,
ni vyema uchunguzi ukifanyika ili kuwatambua watu hao na hatua zaidi
zichukuliwe.
“Ni lazima tufuatilie na vyombo vyetu vya sheria vituambie ni kina
nani hao, vinginevyo hatuna nchi. Tukubali hawa watu wabebe mizigo yao,
hakuna CCM ya wezi, ila kuna wezi ndani ya CCM, hivyo wezi ni lazima
wabebe mizigo yao,” alisema.
Alisisitiza kwamba ripoti hiyo ya PAC inatakiwa kuheshimiwa na kwamba
hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuihoji uhalali wake kwa kuwa inatokana na
kamati maalumu inayotambuliwa na Bunge iliyokusanya taarifa kutoka kwa
vyombo vinavyoaminika vya Serikali, ambavyo ni Takukuru na CAG.
Credit:Mtanzania
Credit:Mtanzania
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment