Wito kwa Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: KUHAKIKISHA UWAJIBIKAJI KAMILI NA PESA ZA UMMA ZINARUDISHWA
Sisi wananchi wa Tanzania:
Tukiwa ni wapiga kura wa majimbo mbalimbali nchini Tanzania, tumechukua jukumu leo kutoa wito kwa wabunge na Rais wa JMT kuhakikisha kuwa uwajibikaji wa hali ya juu unafanyika na wahalifu waliokwapua pesa za umma za Tegeta Escrow mwezi wa 12, mwaka 2013 wanazirudisha mara moja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Uwajibikaji tunaotaka kuuona ni pamoja na:
Wahusika wote wakiwa ama watumishi wa serikali au mawaziri wafukuzwe kazi au kujiuzulu mara moja.
DPP afungue mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu huu na wanufaika wote wa pesa za Tegeta Escrow.
Pesa zirudishwe hata ikitakiwa kwa kuwafilisi wanufaika wa pesa hizi.
Hii ni sehemu muhimu ya wajibu wetu kama raia waaminifu, wenye nia njema ya kuchangia mawazo bora yatakayotuletea uwazi na uwajibikaji nchini kwetu.
Kukaa kimya kwenye jambo ambalo tunaliona linaangamiza taifa na wananchi na kunachangia kuturudisha nyuma kimaendeleo.
Tunataka uwajibikaji kamili na pesa za Tegeta Escrow zirudishwe mara moja
KWA SABABU:- Kutokana na taarifa tulizopokea kutoka vyanzo vinavyoaminika kuhusu ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG); imedhihirika kuwaTANESCO ilikuwa na haki ya kulalamika kuwa ilikuwa ikitozwa na IPTL gharama za uendeshaji (capacity charges) zaidi ya kile kilichokuwa stahili (over charging). Gharama za kukotoa ‘capacity charges’ zilitokana na gharama za mwanzo za uwekezaji pale IPTL, kwa makusudi IPTL iliziongeza gharama hizo kinyume na ukweli na mkataba wake na Tanesco.
KWA SABABU:- Account ya Tegeta Escrow ilifunguliwa mwaka 2006 katika Benki Kuu (BoT) kwa mujibu ya maamuzi ya mahakama ya usuluhishi iliyoshauri kuwa badala ya kulipwa IPTL pesa zile zitunzwe na Benki kuu (escrow account) hadi pale mgogoro utakapopatiwa ufumbuzi na mahakama ya kimataifa ICSID. Ufumbuzi huu ni uamuzi wa ama kukubali kiwango cha capacity charges walichokuwa wakidai IPTL au kukataa na kutumia kiwango ambacho Tanesco walikuwa wakidai. Kwa mazingira ya kutatanisha pesa zote za Escrow zililipwa kwa IPTL mwezi wa 12, mwaka 2013 kabla ya hukumu ya ICSID iliyotelewa mwezi wa 2, mwaka 2014. Hivyo ulipaji huu ulikuwa kinyume cha sheria na makubaliano ya Escrow. (The Citizen)
KWA SABABU:- Ulipaji huu ulio kinyume na sheria, na ulifanywa huku wahusika kutoka serikalini wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, maafisa wa TANESCO, BoT, TRA wakiwa na ufahamu na kushiriki katika mchakato huu wa kihalifu.
KWA SABABU:- Uchunguzi wa PCCB umepata wanasiasa wakiwemo wabunge, mawaziri, majaji na viongozi wengine wa serikali wakishirikishwa katika ‘mgao’ wa fedha hizi tena kwa viwango vya kutisha hadi mabilioni.
KWA SABABU:- Bodi ya shirika la TANESCO haikutimiza wajibu wake na kusababisha ulipaji wa fedha za Tegeta Escrow kinyume na utaratibu, makubaliano na sheria na hivyo kuisababishia TANESCO hasara ya shilingi 321 bilioni .
UWAJIBIKAJI KAMILI TEGETA ESCROW!
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment