Baadhi ya majina yanayotawala mjadala wa uchaguzi mkuu mwaka 2015
Makosa Katika Mchakato wa Kutafuta na Kupata Viongozi wa Kisiasa Tanzania na Suluhisho Lake
SEHEMU YA TATU
Katika sehemu
ya kwanza na ya pili ya makala hii, nilitoa utangulizi wa jumla kwa
kuonesha shida kubwa ya uongozi tuliyonayo katika maeneo mbalimbali ya
nchi yetu. Nilieleza jinsi "siasa" imekua ndiyo jambo muhimu zaidi
kuliko mengine yote kwenye jamii na kudhoofisha maeneo mengine.
Nilieleza kwa undani kwa nini tuko tulipo na aina ya uongozi tulionao.
Nilijenga hoja kuwa nchi yetu haina (na huenda haijawahi kuwa) na mfumo
imara, mpana na wa kudumu wa kuandaa viongozi wenye kubeba maono makubwa
ya nchi yaliyo juu ya maendeleo ya mtu binafsi, chama chake cha siasa
au taasisi nyingine yoyote ile ya umma au ya kijamii. Nilionesha ni kwa
jinsi gani kukosekana kwa mfumo huu imara wa uongozi kumedhoofisha hata
uwezo wa kurithishana maono, mwelekeo, majukumu na madara katika nchi
yetu. Naomba uendelee kusoma sehemu ya tatu:
TUMERUHUSU MFUMO UTUTENGENEZEE VIONGOZI HATARI NA SASA WANATUMALIZA SISI WENYEWE
Sayansi ya
asili, inatufundishwa kuwa vitu viwili haviwezi kuwa kwenye sehemu moja
kwa wakati mmoja. Ni lazima kimoja kiondoke ndipo kingine kichukue ile
nafasi. Unapokua na ndoo imejaa maji na ukawa unataka ndoo hiyohiyo
uijaze maziwa, unalazimika kwanza kuondoa maji hayo ndipo ujaze maziwa.
Wanaoamini katika Mungu wanajua pia kwamba sheria ya imani inasema
huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja maana kwa kufanya hivyo
unaweza kujikuta unamheshimu mmoja na kumpotezea mwingine. Hivyo ni ama
unaamini bwana mmoja na kumpotezea mwingine lakini huwezi ambatana na
wote wawili. Hali kadhalika, sheria ya asili inatuonesha kwamba hakuna
mahali ambapo kuna uwazi (vacuum) na kama hakuna kabisa kitu cha
kuonekana kwa macho basi kuna hewa. Na wenye imani za kidini wanaamini
kwamba kila mtu kuna kitu anachoamini kwani kwa asili mwanadamu hajioni
amekamilika bila nguvu ya ziada iliyo juu yake. Hata wanaosema hawaamini
katika Mungu, bado kuna mambo wanayaamini katika huo upagani au
kutokuamini kwao.
Kama
nilivyoelezea kwenye makala zilizopita, nchi yetu haina mfumo wa
kueleweka wa kuandaa na kupata viongozi wa kisiasa. Hata hivyo viongozi
ni lazima wawepo katika jamii bila kujali wanafaa au hawafai; ni wazuri
au ni wabaya; wameandaliwa au wamejiandaa; wamewekwa au wamajiweka.
Ulazima huo na ukweli kwamba kumekua na ombwe la kutokua na mfumo wa
uongozi unaotoa mwelekeo kuonesha ni wapi taifa linatakiwa kwenda,
kumetoa upenyo wa mifumo mingi mingine kujitokeza na kujiimarisha hadi
kufikia kiwango cha kujiendesha kitaasisi. Hata pale ambapo tumejitahidi
kuonesha kwamba tuna mfumo na tuna viongozi wazuri, ombwe hili limekua
wazi na dhahiri na mara nyingi waovu wameshinda wema na mfumo wa uongozi
mbovu umeuzidi nguvu mfumo wa uongozi wenye malengo. Hii ni kwa sababu
tumeacha mfumo hatari ukue miongoni mwetu na sasa tumejikuta katika
changamoto ya kutumikia mabwana mawili na huku bwana mmoja akiwa ni
katili na asiye na huruma nasi.
Nchi yoyote
duniani inapofikia mahali vyombo vyake vya ulinzi na usalama vinashindwa
kuonesha uwepo na mamlaka yake, cha kwanza kujidhihirisha ni uwepo wa
makaundi yanayotishia amani, usalama na uimara wa nchi (stability)
ambapo hupelekea kudorora kwa usalama wa raia na mali zao. Kwa kawaida
hujitokeza makundi ya wezi, mafisadi, majambazi, majangili, wabakaji,
vibaka, na wengine kama hao ambao wanajiimarisha katika jamii na
kutekeleza matendo yao bila hofu. Kunapokua na ucheleweshaji zaidi wa
serikali na vyombo vyake kujiimarisha, makundi haya hufikia kiwango cha
kuwa taasisi zenye nguvu na hata kujijengea himaya za utawala rasmi. Kwa
mfano:
- Miaka kama miwili iliyopita, nchini Mexico kulikuwa na mbabe mmoja wa dawa za kulevya ambaye siyo tu alijiimarisha na kundi lake kubwa, bali alijiundia utawala na wananchi walimtambua na kumtumikia kama kiongozi katika eneo ambalo alikua ameweka mskani yake. Serikali ilipoamua kupambana naye kwa kulivamia eneo la mji alilokua anaishi, ilikua ni vita ngumu sana ya wiki kadhaa na walikufa watu wengi ikiwa ni pamoja na wanajeshi wa serikali wenye silaha nzito.
- Kuibuka kwa makundi hatari kama Al Shabab, Al Qaida, Boko Haram, Mungiki, Mafia, na mengine yanayotingisha nchi mbalimbali na dunia, kumechangiwa na nchi kukosa uongozi wenye maono na maslahi mapana ya kuhakikisha usalama wa kitaifa.
- Kukosekana kwa mfumo imara wa uongozi kwa nchi kama Libya, Iraq, Syria, Lebanon na nchi zingine, ndio kumeibua makundi ya wapiganaji na wababe wa kivitawanaoisnyia dunia usingizi.
Tanzania kama
nchi tumeshindwa kuwa na mwelekeo wa pamoja kama taifa na hivyo kukosa
kuwa na utaratibu wa kuandaa viongozi wa kutuongoza huko tunakokwenda
(ambako hatukujui kwa sasa). Kwa kufanya hivi, tumeruhusu mifumo mingine
ijiinulie maono yao na viongozi wa kuyabeba. Jambo hili ni hatari sana
na ndilo limefanya mchakato mzima wa upatikanaji wa viongozi wa kisiasa
kuwa soko huria lisilokuwa na mwenyewe. Yameibuka makundi ndani na nje
ya vyama vya siasa na kupandikiza maono yao ambayo wametuaminisha kuwa
ni maono ya kitaifa na kisha kuweka viongozi wa kuyasimia. Wameibuka
watu binafsi kupitia makundi yanayotambulika kama vile vyama vya siasa
na makundi ya kidini na kujiingiza kwenye uongozi wa kisasa kwa malengo
binafsi na mara nyingine mbali sana hata na mtazamo wa makundi
wanayosema wanayawakilisha.
Ombwe la
kukosa mfumo wa kuandaa viongozi wenye maono ya nchi, ndilo limefanya
siasa kuwa mradi wa uwekezaji kwa kila anayejisikia: kuwa uwekezaji
wenye masharti nafuu sana na ulio na kila aina ya uwezeshwaji na
misamaha ya kodi yasiyofuata taratibu na sheria za nchi. Ombwe hili
limebinafsisha dhana nzima ya uongozi wa nchi na kupandikiza picha isiyo
sahihi kwa wengi juu ni nini hasa maana ya uongozi na majukumu yake.
Tunaendeshwa na Majina
Mfumo huu,
umeruhusu baadhi ya watu kwa malengo na maono yao na makundi
wanayoyaongoza kututengenezea maono; kutuchongea viongozi na
kutushawishi kuwa ni wema na waadilifu wenye uwezo wa kututoa Misri na
kutupeleka kwenye nchi ya ahadi. Pale ambapo makundi yamekosa nguvu za
kutosha kutuchagulia viongozi, hata watu binafsi wenye uwezo wa kifedha
wameibuka na kufanya uongozi ni biashara. Watu hawa wanawekeza fedha na
mali zao katika kuwahonga na kuwanunua wananchi ili kujitafutia uhalali
wa kuwaongoza nje ya matakwa na maslahi ya wananchi husika.
Tunagharimika kukuza majina badala ya uongozi:
- Mojawapo ya viashiria vikubwa vya mfumo mbovu wa uongozi ni pale ambapo taifa linapongelea uongozi wa nchi, linajikuta linajadili na kujenga hisia zao katika kuongelea majina ya watu na makundi badala ya dhana ya uongozi na maono ya nchi. Tatizo hilo huwa kubwa zaidi tunapojikuta tunajipa kazi ya kujadili, kuyakuza na kuyatafutia heshima majina badala ya kukuza na kuyatangaza maadili, uwajibikaji, na mwelekeo wa taifa.Tunajadili ni mgombea au mtajwa gani ni maarufu kuliko mwingine; nani ana pesa kuliko mwingine; nani amewahi kufanya nini ukilinganisha na mwingine; na nani ana mke/mume mzuri kuliko mwingine; nani ana watu wengi nyuma ya harakati zake;nani ana sura nzuri zaidi; na nani anaungwa mkono na kiongozi gani mkubwa wa nchi. Tunachukua majina au jina la mtu fulani na kuliweka kuwa kiwango cha juu na kipimo cha aina na uhitaji wetu wa uongozi, sio tu ni hatari kwetu kama taifa, bali ni kiwango kikubwa cha kufilisika kimaono na mtazamo kama jamii.
- Kuendeleza mjadala wa majina katika kuelekea uchaguzi mkuu ni kuzima na kunyamazisha jitihada na harakati za kuibua watu wenye vipawa vya uongozi na maono sahihi kwa taifa letu. Tunapoutazama mjadala wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa miaka kadhaa sasa, tumejikuta katika mjadala ya majina na kuendeshwa na hisia za majina na makundi yao badala ya nini matarajio na maono yetu kama taifa.
- Katika mazingira yaliyoko ya kujadili majina na makundi ya watafuta uongozi, ni ngumu sana kupata mwanya wa kuona watu wanaoweza kusaidia nchi nchi yetu. Hatutaweza kuwaona wala kuwasikia watu sahihi wa kutuongoza maana wameshajengewa mazingira ya kunyamazishwa.
- Kwa kuendelea kujadili majina na makundi yao, tunakua sehemu ya kujenga ufalme na ngome zao na hivyo kujiimarisha zaidi na kujihakikishia kuongoza nchi yetu kwa mitazamo na maono yao ambayo mwisho wa siku wanakua kongwa na mzigo kwa wananchi.
- Tunazuia nafasi kwa jamii kuweza kujadili kwa mapana matakwa ya kiuongozi na mwelekeo wa taifa wanalolitaka
Kwa kuyasema
haya, sina maana kwamba hakuna viongozi wazuri na wenye maono ya kitaifa
miongoni mwa majina yanayotajwa; la hasha! Ninachosema ni kwamba, ni
hatari sana kuweka majina mbele ya vigezo stahiki katika kutafuta na
kupata viongozi wa kisiasa kwa taifa letu. Kiuhalisia ilitakiwa sifa,
vigezo, maono na uhitaji wa viongozi kwa nchi yetu ndio viibue majina ya
wanaostahili kuingia kwenye vigezo hivyo na sio kinyume chake.
Tukitanguliza vigezo, tusingepata changamoto ya majina kwani majina
yasiyofaa yangejiengua yenyewe na yasingejitokeza, na majina ya
waliobeba vigezo yangejitokeza au kutafutwa na wanachi.
Kwa kuwa
tumekosa mwelekeo wa pamoja kama taifa, moja kwa kwa moja tumejikuta
tumeingia katika changamoto ya kuruhusu mifumo hatari ya kutuangamiza
kutuongoza. Pamoja na kwamba hatujaingia katika mapambano ya vita kwa
maana ya silaha, lakini ukweli ni kwamba tuna mifumo na watu binafsi
hatari sana ambao wamechomoza na kupata uhalali wa kutuongoza kwenye
taifa letu. Watu hawa hawana huruma na watanzania; hawana huruma na
rasilimali zetu; hawana huruma na mjane; hawana huruma na watoto
maskini; hawana huruma na usalama wetu. Wanatuaminisha usiku na mchana
kwamba wako kwa ajili yetu, lakini hali halisi tunayopitia kama taifa
katika ngazi mbalimbali, inawakana na kuonesha ni nini hasa
wanachokisimamia.
Katika
mijadala kadhaa ya kitaifa ambayo imekua ikiendelea kwa miaka kadhaa
hasa katika eneo la maslahi ya taifa, rushwa, ufisadi na kukosa maadili,
utaona ni kwa jini gani wale wanaojiitga viongozi wetu
wanavyotofautiana katika kuutafsiri ukweli. Viongozi wetu hawana maana
zinazofafa za ufisadi; hawana maana inayofanana ya uongozi mbovu; hawama
maana inayofanana ya rushwa; na wata tafsi zinazokinzana kuhusu
utumishi wa umma na uhifadhi wa rasilimali za nchi. Watu hawa, wana
tafsiri zinazobishana kuhusu usalama na amani ya nchi.
Tumenyamaza na
tumekataa kujishughulisha kama taifa kuwa na mwelekeo; madhara yake ni
tumeruhusu kuibuka kwa viongozi wa kututafuna na kutungamiza kabisa; na
sasa tunavuna tunachoendelea kupanda.
Katika sehemu
ya nne ya makala hii, nitaanza kutoa baadhi ya mapendekezo ya nini cha
kufanya kama taifa ili kukabiliana na changamoto zinazotukabili.
Nitajaribu kuweka mapendekezo yanayohitaji utekelezaji wa muda mfupi na
yale ambayo ni muda mrefu kwani utekelezaji wake ni mtambuka na kuhitaji
muda wa utekelezaji wake.
Nitapenda kusikia maoni yako na unaweza kuniandikia kupitia barua pepe yangu ambayo ni mmmwalimu@gmail.com.
Mwalimu MM
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment