Monday, December 1, 2014

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 16 NA 17 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 29 NOVEMBA, 2014



I:          UTANGULIZI 
                                   
a)              Masuala ya jumla

Mheshimiwa Spika,
1.            Leo tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Sita na Kumi na Saba wa Bunge lako Tukufu.  Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.

Mheshimiwa Spika,
2.             Mkutano huu ulijumuisha kujadili kazi kubwa zifuatazo:

Kwanza: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/2016;

Pili:                 Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 [The Tax Administration Bill, 2014];

Tatu:              Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani wa Mwaka 2014 [The Value Added Tax Bill, 2014];

Nne:               Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 [The Public Private Partnership (Amendment) Bill, 2014]; na
Tano:             Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2014].

Aidha, ni hivi mapema leo Miswada 11 ya Sheria ya Serikali kuhusu mambo mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.

Mheshimiwa Spika,
3.            Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016. Maoni na Ushauri tuliopokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge tutauzingatia wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2015/2016. Vilevile, niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria niliyoitaja hivi punde.

b)            Maswali
Mheshimiwa Spika,
4.            Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya Papo Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.  Aidha, Maswali 18 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.



c)         Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
5.            Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa tarehe 17 Novemba, 2014 nilipata fursa ya kutoa Kauli ya Serikali kuhusu Mgogoro kati ya Wakulima na Wafugaji Wilayani Kiteto. Aidha, baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri walipata nafasi ya kutoa Kauli mbalimbali za Serikali kama ifuatavyo:

i)          Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu taarifa zilizotolewa na Vyombo vya Habari za shutuma dhidi ya Serikali za China na Tanzania kujihusisha na Biashara Haramu ya Pembe za Ndovu na ile inayohusu Kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa Mwaka 2007;
ii)         Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu Hali ya Dawa Nchini na Matibabu ya Saratani Nchini; na

iii)        Kauli ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu Mwenendo wa Soko la Nafaka na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo.

Maazimio

Mheshimiwa Spika,
6.            Tarehe 7 Novemba, 2014  Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili na kupitisha Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa  Anne  Semamba Makinda (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  kwa  kuchaguliwa kuwa  Rais  wa Mabunge  ya  Nchi  Wanachama  wa Jumuiya ya  Maendeleo  ya  Kusini  mwa  Afrika (SADC-PF). Aidha, katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata pia fursa ya kujadili na kuridhia Maazimio mengine yafuatayo:

i)             Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya, Jumuiya ya Afrika Mashariki;

ii)            Azimio la Bunge la Kufuta na Kusamehe Madai au Hasara itokanayo na Upotevu wa Fedha na Vifaa vya Serikali kwa Kipindi Kilichoishia tarehe 30 Juni, 2011;          
iii)        Azimio la Bunge la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi [The East African Protocol on Cooperation in Defence Affairs]; na

iv)        Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Usalama wa Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari katika Mwambao wa Bara ya Mwaka 1988 [The Protocol for the Suppression of Unlawful Acts Against the Safety of Fixed Platforms located on the Continental Shelf – SUA, 1988].
           
e)         Taarifa Maalum za Kamati
Mheshimiwa Spika,
7.            Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, Waheshimiwa Wabunge walipokea Taarifa Maalum ya Kamati ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee - PAC) Kuhusiana na Miamala iliyofanyika katika Akaunti ya “ESCROW” ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Mheshimiwa Spika,
8.            Naomba nitumie fursa hii, kwanza kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kuruhusu Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha Taarifa hii Maalum kwenye Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wao wa kina na Mapendekezo yao kama yalivyowasilishwa katika Mkutano huu. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliozungumza kwa niaba ya Serikali nzima kutoa maelezo yaliyolenga kutoa ufafanuzi wa hali halisi ya suala hili la Akaunti ya ESCROW ya TEGETA na pia kujibu baadhi ya Hoja za Kamati.

HAPA AMEONGELEA MASUALA YA ESCROW ACCOUNT.

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

a)            Maandalizi ya Kupiga Kura tarehe 14 Desemba, 2014
Mheshimiwa Spika,
9.             Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo ni wa kawaida na unahusisha Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba hadi sasa maandalizi ya Msingi kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika yamekamilika.

Mheshimiwa Spika,
10.         Ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanikiwa, maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi yalifanyika kupitia Vikao vya Wadau mbalimbali ili kupata maoni, mapendekezo na ushauri ambao umesaidia katika kuboresha Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wadau walioshirikishwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu; Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI).

b)            Uandaaji wa Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2014
Mheshimiwa Spika,
11.         Katika maandalizi ya awali, orodha ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji iliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 22 Agosti, 2014 lenye Tangazo la Serikali Namba 300 kwa Halmashauri za Miji na Tangazo Namba 301 kwa Halmashauri za Wilaya. Orodha hiyo imejumuisha Kata, Vijiji na Mitaa. Katika Uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya Vijiji 12,443, Vitongoji 64,616 na Mitaa 3,741 vitahusika kwenye Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika,
12.         Ili kufanikisha Uchaguzi huo, Serikali imekwishaandaa na kuchapisha Vipeperushi, Fomu za Wagombea, Rejesta ya Wapiga Kura, karatasi za kuonyesha Vituo vya Kupigia Kura, Mabango na Matangazo mengine kuhusu Elimu kwa Mpiga Kura. Tayari vifaa hivyo vimepelekwa Mikoani na vingine vinaendelea kupelekwa. Aidha, Masanduku ya Kupigia Kura yameshanunuliwa na tayari yameshasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika,
13.         Kwa vile siku zilizobakia kufikia tarehe ya Kupiga Kura ni chache, natoa Wito kwa Wananchi ambao hawajajiandikisha katika Rejesta ya Wapiga Kura wafanye hivyo bila kukosa. Aidha, Viongozi wa Vyama vya Siasa wawahimize Wanachama wao na Wananchi kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye wajitokeze siku ya Kupiga Kura. Aidha, Wasimamizi wa Uchaguzi wahakikishe vifaa vya Uchaguzi vinafika kwenye maeneo yao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika,
14.         Napenda nitumie nafasi hii kutoa Rai kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa waendeshe kampeni kwa amani na kuepuka maneno ya uchochezi, kubaguana kwa misingi ya ukabila, rangi, udini ama hali ya mtu mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani. Aidha, nawaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wanachama wao, wakishapiga kura wasiendelee kukaa katika Vituo vya Kupigia Kura, bali watawanyike na kusubiri muda wa matokeo.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
15.         Leo nimeona nizungumzie masuala muhimu yanayochangia kusukuma Gurudumu letu la Maendeleo. Kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.  Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu.  Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu.

Mheshimiwa Spika,
16.         Naomba pia nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.

Mheshimiwa Spika,
17.         Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenuAidha, niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2015. Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuvusha salama sote kama tulivyo hadi kuuona Mwaka Mpya wa 2015.  Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 27 Januari, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 18 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika,
18.         Naomba kutoa Hoja.

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!