Saturday, November 8, 2014

“Hatua ya kujifungua inatisha. Ni wanaume wachache ambao wanaweza kushuhudia wenzi wao wakijifungua kisha wakaendelea kuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia,” anaanza kuelezea Dk Matilda Ngarina.

“Ni tukio la kuogopesha. Linahitaji ujasiri wa ziada. Wanaume waliojaribu kushuhudia wenzi wao wakijifungua asilimia 90 wameathirika kisaikolojia,” anasema.

Dk Ngarina ni miongoni mwa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).


Anaeleza baadhi ya athari za kisaikolojia walizopata wanaume hao, zimesababisha wengine kujikuta hawatamani tena kutungisha mimba.

“Wapo wanaume wengine waliochukua uamuzi wa kuomba wake zao wafungwe kizazi, ili kuwaepusha kuzaa tena na wengine walipoteza hamu ya kushiriki kwenye tendo la ndoa,” anasema.

Anasema wapo wengine ambao baada ya kukumbwa na athari hizo walijisalimisha kwa madaktari kuomba msaada, ambapo walikutanishwa na wataalamu wa masuala ya saikolojia na wakarejea katika hali yao ya kawaida.

Dk Ngarina anasema uamuzi wa kuzungumza na wataalamu wa afya mtu anapopatwa na matatizo, ni jambo muhimu kuliko kuruhusu athari ziendelee kutawala.

“Ukweli ni kwamba wanaume wengi hawana desturi ya kushiriki kwenye kliniki ili wapate elimu ya masuala ya afya na uzazi jambo ambao ni muhimu kusaidia kuwa na familia bora,” anasema.

Anaeleza kwa sasa wanaume wengi wanabainika kuwa na matatizo ya uzazi zaidi kuliko hata wanawake, hali ambayo inasababishwa na mfumo wa maisha yao.

Anafafanua kuwa matumizi ya pombe na sigara, kazi za nguvu na joto kali ni miongoni mwa mambo ambayo yanasababisha wengi kupungukiwa na nguvu za kiume.

“Licha ya elimu ambayo tumekuwa tukitoa mara kwa mara kuhusu madhara ya pombe na sigara imekuwa ni vigumu kueleweka kwa wanaume wanaopenda kutumia,” anasema.

Dk Ngarina anasema katika kuhakikishan kwamba wanawavutia wanaume kushiriki kwenye kliniki wanatoa huduma hiyo mchana na jioni.

“Tunatambua wao ndiyo watafutaji wakubwa wa kipato cha familia, hivyo pengine wanakosa muda asubuhi, tumeanzisha muda huo ili waweze kupata muda wa kujua mambo yanayohusu afya zao kwa jumla,” anasema.

Anasema hali ilivyo ni kwamba asilimia 23 ya wanaume wanaitikia wito wa kuhudhuria kliniki kujua afya zao binafsi, pamoja na kufuatilia kwa karibu afya ya wenzi wao.

Mazingira ya kuwavutia wanaume kliniki

Meneja wa Mradi wa ‘Tanzania Men as Equal Partners’ (TMEP), Cuthbert Maendaenda anashauri Serikali kujenga mazingira mazuri ya kuwashirikisha wanaume katika masuala ya afya na uzazi wa mpango kwa jumla, ambayo pia yatawaruhusu kushuhudia wenzi zao wakijifungua.

Anasema kuwa anaamini hatua hiyo ya kuwashuhudia wenzi wao itasaidia kuwashawishi wanaume wengi kuongeza umakini katika suala zima la uzazi.

“Mazingira yaliyopo sasa katika hospitali zetu nyingi yanawafanya baadhi ya wanaume kujitenga, kutoona umuhimu wa wao kushiriki kwenye masuala hayo,” anasema.

Anatoa mfano kuhusu kliniki, imekuwa ni eneo linalotambulika kwamba linashughulikia huduma ya afya ya mama na mtoto.

“Hali hii mimi naona inakuza mfumo dume na inawatenga wanaume wengi kuhudhuria huko, wakiamini kwamba ipo kwa ajili ya afya ya mama na mtoto pekee hivyo hujisikia vibaya kuhudhuria huko,” alisema.

“Mimi naamini kwamba pia hata mama anapokuwa katika hatua ya kujifungua mumewe anapaswa kuwepo ili ashuhudie, hii itawahamasisha wanaume wengi kuwa wajumbe wazuri wa uzazi wa mpango.

Anasema hatua hiyo pia ikitekelezwa itafanikisha mkakati wa taifa wa malezi bora kwa mama na mtoto,” alisema Maendaenda.

“Nina imani na serikali kwamba ikiamua inaweza kutengenezwa miundombinu ya kuruhusu hatua hiyo, ambayo tayari kwenye baadhi ya hospitali nyingine za binafsi inaendelea,” anasema.

Maendaenda anasema hatua hiyo pia itasaidia kuondoa, malalamiko dhidi ya wauguzi kunyanyasa wazazi, kwa sababu huduma nyingine zisizohitaji utaalamu kitabibu kama vile kumpa chai mume ndiye atamhudumia.

“ Kweli kuna wakunga wanawadhalilisha wajawazito wakati wa uzazi kwa maneno ya kashfa, naamini mume akiwepo pale, hakutatokea mambo kama hayo, atashiriki kikamilifu kumwezesha mama kujifungua salama,” anasema Maendaenda.

Anasema pia wanaume kwa jumla wanapaswa kupata elimu ya uzazi, kwani wapo ambao wana matatizo ya uzazi, lakini wamekuwa wakiwashushia lawama wake zao, kutokana na hali ya mfumo dume.

Alitaja baadhi ya kazi ambazo zina mazingira ya kuua uwezo wa mwanaume kutungisha mimba, kuwa ni pamoja na kuendesha pikipiki, upishi na udereva wa magari ya safari ndefu.

“Kwa kawaida kiwango cha joto ambalo ni nyuzi 35 yaani linakuwa limeshuka nyuzi mbili za joto la kawaida la mwili ndiyo linatakiwa kuhifadhi sehemu za siri za mwanaume.”

“Lakini kazi hizo huwafanya wanaume wanaozifanya kuruhusu sehemu zao za siri kupata joto kubwa zaidi,” alisema.

Alisisitiza kuwa pia baadhi ya nguo za ndani zilizotengenezwa kwa malighafi ya polyester na mavazi ya kubana ni hatari kwa mfumo wa uzazi wa mwanamume.

Anasema mavazi hayo husababisha kiwango cha joto kuwa kikubwa zaidi ya kile kinachotakiwa, hivyo kuharibu hifadhi halisi ya kifuko cha mbegu za uzazi.

Mjamzito Zulfa John anasema amekuwa akijisikia vibaya pale anapowahi kufika kliniki, lakini wauguzi husika huwapa kipaumbele wenzao waliofika na waume zao ili wawahi kuondoka.

“Ukifikiria huwezi kukasirika ila maumivu yananipata kwamba mume wangu hataki kabisa kunisindikiza kliniki, lakini ananipa fedha ya kutosha kunifanya niende kliniki na kurudi.”

Samson Joshua anasema kuwa anatambua hali ya ujauzito ilivyo ngumu hivyo anajitahidi kuwa karibu na mkewe aitwaye Aneth, ili kumhakikishia yupo pamoja naye kwa kila hali kama alivyoapa kwenye kiapo cha ndoa.

“Niliapa nitakuwa naye kwa shida na raha, sasa ujauzito unabeba yote hayo mawili kwa wakati mmoja yaani kuna shida tunakumbana nazo, lakini pia ni raha kutarajia kupata mtoto, hivyo najisikia poa kuongozana naye kliniki,” anasema Joshua.


POSTED BY Mwananchi: ‘Kushuhudia mke akijifungua kumeathiri wengi’

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!