Sunday, November 9, 2014



Wakipata chakula cha mchana baada ya wananchi wa Ilemi kuwachangia. 

Wanachama wa CHADEMA walichangishana na kuapata debe 7 za mahindi na fedha taslimu shilingi 20,000/= Wanachuo 48 wa Chuo cha Kilimo cha Nice Dream kilichopo mtaa wa Mapelele Kata ya Ilemi Jijini Mbeya wanakabiliwa na ukosefu wa chakula baada ya uongozi wa Chuo hicho kuwatelekeza na kutokomea kusikojulikana.

Hayo yamebainishwa na Diwani wa Kata ya Ilemi Mheshiwa Furaha Mwandalima baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachuo hao na kufika Chuoni hapo na kujionea hali halisi.

Mwandalima alichukua hatua za haraka za kumtafuta Mstahiki Meya ambaye alimshauri kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wiliya ya Mbeya ili kupata mustakabali wa suala hilo.

Hata hivyo lilitolewa agizo la kuorodhesha majina ya wanafunzi na mahali wanakotoka ili kuwarudisha makwao na Chuo kifungwe kutokana na Chuo hicho kutosajiliwa rasmi na kwamba kilikuwa kinaendeshwa kijanja na wanachuo hao wamelipa malipo ya awali zaidi ya shilingi laki tano.

Zaidi ya wanafunzi 40 wanatokea Mkoa wa Kagera na wawili wakitokea mkoani Mara ambapo wawili wanatokea wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya hali mmoja akitokea Mkoa wa Dar es Salaam.

Mmoja wa wanachuo aliyejitambulisha kwa jina la Jenitha Carist alisema waliletewa taarifa na wakuu wa shule walizokuwa wakisoma baada ya kumaliza Kidato cha Nne mwaka uliopita kuwa wamechaguliwa na serikali kusomea Kilimo Mkoani Mbeya, lakini walipofika walishangazwa na hali waliyoikuta na kwamba walipofuatila kwenye mtandao walibaini chuo hakikuwa kimesajiliwa katika Baraza la Vyuo.

Walipoutafuta uongozi wa Chuo hicho, uongozi ulianza kupiga chenga, ndipo walikwenda kutoa taarifa Polisi na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Uongozi wa Wilaya umeanza hatua za kumtafuta mmiliki ili aweze kutoa majawabu.

Hali ilikuwa tete siku ya Jumamosi ambapo baadhi ya wanachuo walizirai kwa njaa na kulazimu Diwani Furaha Mwandalima kuchangisha kwa dharura na kufanikiwa kukusanya debe nne za mahindi na maharage debe moja na kuandaa mlo wa mchana.

Baadhi ya majirani walishindwa kujizuia kwa kuangua kilio kutokana na hali mbaya kwa baadhi ya wanachuo ambapo baadhi walilazimika kuandaa uji ili kutoa msaada wa haraka.

Kwa upande wake Diwani Mwandalima amemshukuru Mstahiki Meya Athanas Kapunga na Mkurugenzi kwa kuhudi zao ili kuwafanya wanachuo hao wafarijike hasa kutokana na wengi wao kutokuwa na na ndugu na wanatoka mikoa ya mbali.

Mwandalima ametoa wito kwa wakazi wa Mbeya kutoa mchango wa hali na mali ili kuokoa maisha ya wanachuo hao. Pia amewashukuru wakazi wa Ilemi kwa kuchangia chakula na mahitaji mengine kwa wanachuo hao.


 Chuo hiki kilizinduliwa mwaka huu na Mhr .Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu

Moja kati ya mabweni ya chuo hicho ambapo hulala chini wanafunzi kati ya 10 mapaka 15 kweli taasisi zinazihusika na ukaguzi wa vyuo hivi zipo? 

Hii ndilo shamba darasa la chuo hicho



0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!