Sisi Viongozi wa Mila, Kisiasa, Wawakilishi wa Wanawake tumesikitishwa
sana na Taarifa ya uongo aliyoitoa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Lazaro Nyalandu juu ya ukweli wa Mgogoro wa Loliondo. Ifuatayo ni
ufafanuzi wa hali halisi kinyume na Waziri alivyodanganya Dunia kupitia
BBC tarehe 19/11/2014 na Gazeti la leo la Mwananchi
- Kwamba eneo la Loliondo halina Wamaasai 40,000 watakaoadhirika endapo Serikali itatoa tamko Wakati wowote sasa:
Jibu: Idadi ya wakazi katika eneo la km za mraba 1,500 ambavyo ni vijiji
vya Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Arash, Maaloni,
Olorien/Magaiduru, Piyaya na Malambo ambavyo vina jumla ya wakaazi
57,532. Kwa mujibu wa sensa ya Taifa ya watu na Makazi ya 2012 kama ilivyo kwenye jedwali hapa chini.
SN
|
Kata
|
Idadi ya watu
|
1
|
Arash
|
7,841
|
2
|
Olosoito/Maaloni
|
4,353
|
3
|
Oloipiri
|
4,114
|
4
|
Soitsambu
|
10,956
|
5
|
Ololosokwan
|
6,557
|
6
|
Piyaya
|
5,303
|
7
|
Malambo
|
8,923
|
8
|
Olorien- Magaiduru
|
9,485
|
9
|
Orgosorok
|
1,521
|
10
|
Engusero Sambu
|
12, 268
|
Jumla
|
71, 321
|
Vijiji viwili (Engusero sambu na Orgosorok) venye idadi ya watu 13,789
hawana makazi katika eneo la mgogoro lakini ni watumiaji wa eneo hilo la
malisho.Hivyo tunathibitisha kuwa watu watakaoathirika eneo hili
likichukuliwa ni 71,321.Hivyo Waziri kusema eneo hilo halina watu 40,000
ni uongo mtupu.
- Kwamba Serikali ya Tanzania haijawahi kuwa na mpango wa kuwaondoa Wamaasai katika eneo la Loliondo:
1992: Serikali ilitoa ardhi ya vijiji vya Tarafa za Loliondo na Sale kwa
Mfalme wa UAE bila RIDHAA ya wananchi na kusababisha mgogoro
unaoendelea mpaka sasa. Kumweka mwekezaji katika ardhi ya jamii bila
ridhaa ilikua ni mpango wa muda mrefu wa kupora ardhi.
2008: Mgogoro huu umechukua sura tofauti baada ya kampuni kuweka
mikakati ya kuchukua ardhi yetu kwa ajili ya uwindaji na kutengeneza
mikataba iliyoridhiwa na viongozi na sio wananchi.
2009: Serikali ilitumia mikataba iliyoridhiwa na baadhi ya viongozi wa
vijiji kufanya opersheni ya kijeshi ambayo iliharibu rasilimali,
ilichoma makazi na kusababisha mtoto moja katika kijiji cha Arash
kupotea mpaka leo. Kijana Ngodidio Rotiken alijeruhiwa kwa bomu na
kupoteza jicho na madhara mengine mengi.
2010: Serikali ilitengeneza RASIMU ya mpango wa Matumizi wa Ardhi ya Wilaya kwa ufadhili wa OBC wa shilingi 157,000,000. Mpango
huo ulitengeneza rasimu ya ramani ya kutenga eneo la Kilomita za Mraba
1,500 kutoka kwenye ardhi ya vijiji. Mpango ulipingwa vikali na
kukataliwa na baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro na
jamii kwa ujumla kwa sababu ya dhana nzima ya kutenga ardhi ya vijiji
bila ushiriki wa wananchi.
2011/12: Serikali kupitia kamishina wa ardhi iliagiza
vijiji vya Ololosokwan na Engaresero kurudisha vyeti vya ardhi ya vijiji
kwa madai kuwa vina migogoro. Madai hayo yalithibitishwa kuwa ya uongo
na yenye hila ya kupora ardhi ya vijiji.
2013: Serikali kupitia Mhe. Waziri wa Maliasili na
Utalii (Mhe. Khamis Kaghasheki) ilitangaza RASMI kutenga eneo la
Kilomita za mraba 1,500 ya ardhi ya vijiji kuwa Pori Tengefu la
Loliondo. Jambo hili lilizua taharuki kubwa ndani na nje ya Nchi na
kutishia usalama kwenye jamii ya Wafugaji na hatimaye kumlazimu Waziri
Mkuu kuingilia kati.
2014: Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro
Nyalandu (Mb) alizuru Loliondo mara mbili kwa nia ya kuhamasisha na
kushawishi madiwani na wenyeviti wa vijiji kukubali pendekezo la
Serikali/OBC kutoa FIDIA ya shilingi Bilioni moja kwa vijiji endapo
watakubali kuachia eneo la kilomita za mraba 1,500. Pendekezo lake
halijakubaliwa hata na viongozi wachache aliyokutana nao.
Tarehe 19/11/2014 wakati wa mahojiano na mtangazaji
wa BBC, Mhe. Lazaro Nyalandu alisema alikwenda Loliondo Kuhamashisha
Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi:
Jibu: Waziri kisheria,
hana mamlaka juu ya kupanga matumizi ya Ardhi ya vijiji na wala
haijawahi kuzungumziwa katika mikutano ya Waziri na Baadhi ya Madiwani
na wenyeviti alipokuja Loliondo. Mipango ya Matumizi bora ya
ardhi za vijiji inaratibiwa na Wizara ya Ardhi na Makazi na sio Wizara
ya Maliasili na Utalii…….. Ni Wizara hiyo hiyo inayoongozwa na Nyalandu
iliyopinga upimaji wa vijiji uliokuwa unatekelezwa na Wizara ya Ardhi na
Makazi mwaka 2013 kwa kuwarudisha ndani ya masaa 24 timu ya wataalamu
wakiongozwa na mpima wa Wizara ya Ardhi Ndg. Isaa Marwa waliokuwa
wameanza zoezi la upimaji.
Katika Mahojiano na BBC tarehe 19/11/2014, Waziri
Nyalandu alisema sio Wamaasai tu wanaishi katika eneo la kilomita za
mraba 1500:
Jibu: Wakazi wa eneo hili ni wafugaji wa jamii ya wamaasai ambao ni zaidi ya 40,000
Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 21/11/2014 Mhe Nyalandu alisema “yaani tunapanga kutumia askari kuwaondoa wananchi kwenye maboma yao na kuyachoma moto…..Huu ni uongo, hakuna mpango kama huo”
Jibu: Kwa kuwa Mhe Waziri
Lazaro Nyalandu yaelekea hana kumbukumbu ya matukio ya Loliondo
tunamrejesha kwenye tukio la mwaka 2009 lililoratibiwa na Wizara ya
Maliasili na Utalii kutumia jeshi la Polisi (FFU) kuteketeza kwa moto
maboma ya wafugaji ya jamii ya Kimaasai zaidi ya 300 katika eneo la
Loliondo.
- Baada ya mkanganyiko huu wa Mhe Nyalandu, sisi viongozi wa Kisiasa, Kimila na Wawakilishi wa wanawake tumedhamiria kumwona tena Mhe. Waziri Mkuu ili kupata uhakika wa mpango huu wa Nyalandu, kwani hatuna imani tena na Wizara ya Maliasili na Utalii. Tumeumizwa na kusikitishwa sana na kitendo cha kushindwa kumwona japo tulipata uhakika wa muda wake wa kutuona (appointment) tarehe 19/11/14.
- Katika sakata hili tunatoa tena kwa mara nyingine ushauri ufuatao kwa Serikali ili kufikia suluhu ya kudumu kwa mgogoro huu:
I. Waziri
Mkuu kutoa agizo lenye masharti ya muda kwa Wazira ya Maliasili na
Utalii kufuta kwa Maandishi Tamko lake kwa vyombo vya habari la tarehe 21, Machi 2013 kama ulivyotuahidi Sept mwaka jana.
II. Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kutengua/kufuta hadhi ya Pori
Tengefu katika vijiji vya Loliondo kwa mujibu wa sheria mpya ya
Wanyamapori ya mwaka 2009 na kuheshimu miliki halali za kisheria kwa
ardhi yetu na mfumo wa maisha yetu usioharibu mazingira.
III. Waziri Mkuu kutoa TAMKO kwa umma wa Watanzania na Dunia nzima kwamaandishi kuhusu Ahadi yake ya tarehe 23/9/13 kwetu kwamba Serikali imeachana na mpango wa
kupora ardhi ya Vijiji vyetu. Aidha tunamwomba Waziri Mkuu kukemea kwa
uzito usumbufu huu tuanoupata watu wa Loliondo toka kwa Wizara ya
Maliasili na Utalii unaojirudia kila Wakati.
IV. Tunaishauri
Serikali kufuta uwindaji katika Ardhi yetu, kwani hauhifadhi
Wanyamapori wala sio rafiki na mazingira, ufugaji na utalii wa picha.
Uwindaji katika eneo la Loliondo ni mpango wa kuwamaliza wanyama katika
ikolojia ya Serenegeti, Ngorongoro na Maasai Mara. Kuendelea kuruhusu
uwindaji katika eneo hili, mgogoro utaendelea na kusababisha madhara
endelevu kwa uhifadhi wa wanayamapori, maisha yetu na ustawi wetu.
V. Tunamwomba Mhe. Waziri Mkuu kutoa maelekezo ya haraka kwa Wizara ya Ardhi na Makazi iendelea na zoezi la upimaji wa vijiji lililohairishwa na Wizara ya Maliasili na Utaliimwezi August, 2013 ili kuharakisha zoezi la kuandaa mipango ya Matumizi ya bora za Ardhi.
VI. Tunamwomba
Mhe. Waziri Mkuu kutekeleza haya kwa muda mfupi uwezekanavyo kwani
tumekuheshimu kwa kuvuta subira kwa mwaka mzima kama ulivyotuelekeza
kwenye Barua yako ya Mwezi Mei mwaka jana “tuwe watulivu na wavumilivu wakati ukishughulikia kilio chetu”. Kama utashindwa kutoa maelekezo hayo ya kutimiza ahadi yako
kwetu, basi hatuna budi kuhamasisha dunia kupitia vyombo vya habari na
kufika Dodoma ofisini kwako kwa maelfu ili utueleze hatma ya Ardhi yetu
na maisha yetu. Japo tunaamini katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya
amani, hata hivyo uvumilivu umetuishia na kamwe ardhi yetu haitaporwa kwa maslahi ya kampuni ya OBC.
Imeandaliwa na:
1.Elias Ngorisa – Mwenyekiti Wa Halmashauri
2. Ibraham Sakai- Mwenyekiti wa CCM Wilaya.
3. Daniel Ngoitiko- Diwani
4. Mathew Siloma- Diwani
5. Tina Timan- Diwani
6. John Kulinja- Kiongozi wa Mila.
7. Mathew Timan- Kiongozi wa Mila
8. Loserian Minis- Mwakilishi wa Wenyeviti wa Vijiji.
9. Kooya Timan – Mwakilishi wa Wanawake
10. Manyara Karia- Mwakilishi wa Wanawake
Imetolewa leo tarehe 21/11/2014, Arusha na Wawakilishi wa Jamii toka Tarafa za Loliondo na Sale.
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment