Monday, November 10, 2014

Vita vimekuwa vikiendeleea nchini Sudan kwa miezi 11 sasa huku maelfu wakiachwa bila makao

Mapigano mapya yamezuka katika majimbo matatu nchini Sudani kusini , siku chache baada ya pande mbili hasimu kukubaliana kumaliza mzozo ambao umekuwepo kwa miezi 11.


Wiki iliyopita, Raisi wa Salva Kiir na Kiongozi wa waasi Riek Machar walikubaliana kumaliza mapigano kufuatia mazungumzo ya siku mbili nchini Ethiopia.

Serikali na Waasi wamekuwa wakinyoosheana kidole kuwa wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika jimbo la Upper Nile,Unity na Jonglei.

Msemaji wa Waasi Brigedia Jenerali Lul Ruai Koang ameishutumu Serikali kwa kuanzisha mashambulizi dhidi yao hasa katika maeneo yenye mafuta katika jimbo la Unity.

Lakini msemaji wa Jeshi Philip Aguer amesema vikosi vya waasi ndivyo vilivyoanzisha mapigano, kisha wao haraka wakajibu mashambulizi.

Mazungumzo yanayoratibiwa na jumuia ya IGAD,ambayo imetoa muda wa siku 15 kwa pande zote mbili kufikia makubaliano kumaliza mzozo.IGAD imetishia kuweka vikwazo ikiwemo marufuku ya kusafiri na usafirishaji wa silaha,ikiwa makubaliano hayatafikiwa kwa kipindi kilichotolewa.

Maelfu ya Watu wameuawa kwenye mapigano ya Sudani kusini na wengine milioni 1.8 wamekimbia mapigano tangu yalipoanza nchini humo katikati ya mwezi Desemba mwaka jana.

POSTED BY BBC

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!