Saturday, November 15, 2014

Shirikisho la soka la Qatar limesema liko tayari kusimamia maandalizi ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (CAN) itakayochezwa kuanzia Januari 17 hadi Februari 8 mwaka 2015, iwapo viongozi wa Emirate watafahamishwa rasmi, amesema Alhamisi Novemba 13 rais wa shirikisho hilo.

Uamuzi huo unakuja baada ya mataifa zaidi ya tano kutoka barani Afrika kukataa kusimamia maandalizi ya michuano hiyo yakidai kuhofia afya za raia wao.

Morocco ambayo ingelikuwa mwenyeji wa michuano hiyo iliomba iahirishwe kufuatia mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola, lakini shirikisho la soka barani Afrika, CAF pamoja na shirikisho la soka dunia FIFA, vilitupilia mbali hoja hiyo.


Rais wa shirikisho la soka la Qatar Sheikh Hamad Ben Khalifa Ben Ahmed Al Thani, amesema hawajapokea ombi rasmi kwa minajili ya maandalizi ya michuano ya kombe hilo.


Ikiwa michuano hiyo itachezwa Qatar, itakuwa mara ya kwanza michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kuchezwa nje ya Afrika.
Sheikh Al Thani anapingana na Naibu wake, ambaye alisema Jumatano wiki hii kwamba michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kuchezwa nje ya Afrika itakuwa haina “umuhimu wowote”.

via RFI

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!