MATUMIZI ya kondomu za kike yamekuwa changamoto kubwa baada ya wanawake mkoani Rukwa kukataa kuzitumia, huku wengine wakibadili matumizi yake kwa kuzivaa kama urembo wa bangili.
Hayo
yalibainika hivi karibuni wakati wa ziara ya siku nne ya timu za
maofisa wa asasi mbili zisizo za kiserikali za Health Actions Promotion
Association (HAPA ) ya Mkoa wa Singida na Resource Oriented Development
Initiative (RODI) mkoani Rukwa. Maofisa hao walikuwa wanatembelea miradi
inayotekelezwa na Mradi ya Ushirikishaji wa Wanaume katika Afya ya
Uzazi na Ujinsi (TMEP) mkoani hapa.
Mkurugenzi
wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Rodi inayohusika na kutoa elimu ya njia
sahihi ya kutumia kondomu ili kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya
Ukimwi (VVU), Gideon Mpina alikiri matumizi sahihi ya kondomu za kike ni
changamoto kubwa mkoani humo.
Alisema
kwa kuwa kondomu hizo zina umbo la bangili, baadhi ya wanawake
wanazitumia kuvaa mikononi kama urembo kinyume na matumizi sahihi ya
kondomu hizo.
“Bangili
za kondomu hizo zimekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake. Wanazivaa
mikononi kama urembo kwani zinapendeza machoni sababu zikipigwa na
mionzi ya jua zinabadili rangi mbalimbali na kuwa kivutio cha aina
yake,” alisema Mpina.
Alisema
imekuwa changamoto kubwa kwa Rodi kwani licha ya kuisambaza bila
malipo, bado baadhi ya wanawake wanazitumia na wengine kuzinunua kutoka
kwa wenzao ili tu wapate bangili.
Rodi pia inatoa elimu kuhusu malaria mkoani hapa kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Manispaa.
Naye
Mratibu na Mfuatiliaji wa Shidepha+ wilayani Nkasi , Anna Laurent
alikiri kuwa wanawake wengi wanakataa kutumia kondomu za kike kwa sababu
wanazozijua wao wenyewe, hivyo kusababisha kondomu hizo kudoda ofisini
kwake.
“Licha
ya kukataa kutumia kondomu hizi za kike, lakini wamekuwa wakichangamkia
kuchukua kondomu za kiume kwa wingi na kusababisha uhaba mkubwa …
mahitaji ya kondomu za kiume ni makubwa kwani zinachangamkiwa na wote,
wanaume kwa wanawake,” alisisitiza.
Kwa
upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga, Dk Richard
Manumba alibainisha kuwa baadhi ya wanawake mkoani humo hawapendi
kutumia kondomu za kike, kwa sababu zinawafanya wasiaminike na wenzao
kwa kuwa baadhi yao wanadaiwa kuzitumia zaidi ya mara moja kwa wanaume
tofauti.
posted by paparazi
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment