Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo
Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekataa maombi ya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000.
Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.
Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu imeshindikana kufanya hivyo.
Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.
Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi kuhusu suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo itakapotengamaa,” alisema Hamad.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh 150,000 kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000 kwa mwezi.
Akizungumzia kikao cha bajeti kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na linatarajiwa kukutana Agosti 5.
Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti kinatarajia kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda na kuwahi Bunge la Katiba.
Aidha, katibu huyo wa BLW alisema kikao hicho kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya Fedha na ule wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka 2014/2015.
Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo mbalimbali.
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment