Walimu wawili wanaojitolea katika
Shule ya Msingi Msali, Kata ya Nyakahura, wilayani Biharamulo, mkoani
Kagera wanatumia vipande vya mihogo mikavu na mkaa kuandikia ubaoni
baada ya kukosa chaki.
Wakizungumza shuleni hapo juzi,
walimu hao walisema hawana chaki za kuandikia na kwamba wanatumia vitabu
viwili vya hesabu na kiswahili kufundishia wanafunzi 200.
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo, Evelina Jeremiah alisema shule hiyo ilianzishwa
mwaka mmoja uliopita kutokana na uwapo wa watoto wengi ambao hawajaenda
shule lakini haijasajiliwa.
Alisema baada ya kuwa na
idadi kubwa ya watoto, wazazi walianzisha banda la kuwafundisha kusoma,
kuandika na kuhesabu hali iliyosababisha kuajiri vijana waliomaliza
kidato cha nne kuwafundisha.
Jeremiah alisema licha ya
kukosa chaki na vitabu, kuna upungufu wa madawati na madaftari kwani
wanafunzi hao hawapati mahitaji muhimu ya shule ukilinganisha na wenzao
wa shule nyingine za Mzani na Nyakahura.
“Tunafundisha
kwa taabu maana hata mshahara tunalipwa na wazazi Sh30,000 kwa mwezi,
lakini kupatikana kwake ni kuvutana na kutufanya tuishi maisha ya
ombaomba,” alisema.
Naye Mwalimu Robert Mussa alisema matatizo mengine ni kuvuja kwa
jengo linalotumika kama darasa wakati wa mvua na kuathiri ufundishaji.
Diwani
wa Kata ya Nyakahura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Biharamulo, Apolinary Mugarula alikiri kuwapo kwa shule hiyo na
kwamba, ilianzishwa kinyemela na wafugaji wa eneo hilo bila usajili.
Mugarula
alisema tayari uongozi wa kata umetoa maagizo kwa walimu wa shule hiyo
kufuata chaki Shule ya Msingi Mzani na vitabu vya kufundishia, wakati
utaratibu wa kuisajili ukiendelea.
Alisema matatizo ya shule hiyo ni mengi hasa madarasa, vyoo, madawati na nyumba ya walimu.
Diwani
huyo wa Kata ya Nyakahura aliongeza kwamba, kubwa zaidi ni kuwaweka
walimu waliopitia mafunzo chuoni badala ya vijana wasiotambua maadili ya
utumishi kitaaluma.
POSTED BY PAPARAZIHURU...
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment