Friday, November 14, 2014

Museveni akiwa kulia mwa Mugabe 

Habari kubwa hivi sasa barani Afrika ni mapinduzi ya umma yaliyofanyika Burkinafaso, makala haya ni mtazamo wangu kuhusu kitakachojiri kusini mwa jangwa la sahara kuelekea 2030, mtazamo huu umejikita katika kutathimini matukio yanayoendelea kusini mwa jangwa la sahara na hali ya kisiasa kwa ujumla, fuatana nami katika maandishi haya ya kusisimua;

Kusini mwa jangwa la Afrika si salama

Dalili za wazi zinaonyesha kuwa nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara zipo katika hali mbaya zaidi ya nchi za kiarabu zilizopinduliwa kama Misri na Tunisia , halikadhalika kwenye mataifa hayo ya kusini mwa jangwa la sahara kuna ukosefu mkubwa zaidi wa ajira hivyo kufanya idadi kubwa ya vijana kuwa wazururaji kuliko Burkinafaso ambayo imepinduliwa hivi karibuni. Sasa ikiwa hali iko hivi kwanini viongozi wa mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara hawachukui tahadhari? Kwa nini wanazidi kujisahau?
Viongozi wengi wa kusini mwa jangwa la sahara wanategemea kuudhibiti upinzani kwa msaada wa vyombo vya dola mfano mzuri ni hujuma kubwa dhidi ya viongozi wa upinzani kwenye baadhi ya mataifa yanayounda jumuiya ya Afrika Mashariki. Tatizo kubwa la marais hawa nikule kudhani kuwa vyombo vya dola vinaweza kuudhibiti umma, wanapaswa kujifunza kwa makini maana halisi ya nguvu za umma na athari zake kwa muktadha wa siasa za taifa lolote ulimwenguni, yatosha kuzingatia kuwa umma haujawahi kushindwa.

Vyama vingi tawala vitakataliwa

Kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi vyama vingi tawala vitakataliwakatika mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara. Kuanzia miaka ya 1990 vuguvugu la vyama vya upinzani limeweza kuving’oa vyama tawala kadha wa kadha mifano ya UNIP Zambia, KANU Kenya na PDS Senegal hapa pia usisahau kuangushwa kwa chama cha UMD cha Fredrick Chiluba huko Zambia kilipopoteza kwa Michael Satta wa PF.

Angukohili la vyama tawala halikwepeki hasa kwa kuzingatia udhaifu wa vyama hivyo katika kushughulikia shida za wanyonge ikiwamo bei za mazao, ajira na kupanda kwa gharama za maisha, utegemezi mkubwa wa nchi za kiafrika kwa wawekezaji kutoka nje ,uwekezaji ambao umeshindwa
kuondoa umasikini una kila dalili mbaya kwa vyama vya ANC Afrika Kusini, FRELIMO Msumbiji na CCM Tanzania, kuelekea 2030 vyma hivi vimezidi kupunguza idadi ya kura huku upinzani ukizidi kushika kasi kwenye nchi zao.

Marais ving’ang’anizi watang’olewa kabla ya 2030

Mwanahistoria Jovitus Mwijage katika kitabu chake “Major Events in African History” akielezea kushindwa kwa viongozi wengi waliotwaa madaraka kwa njia za mapinduzi mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzano mwa miaka ya 1990 , katika ukurasa wa 308 anasema “Under the auspices
of the constitutions made by them (African dictators), the ballots could not change the existing leadership; therefore, the barrel of the gun eventually became answer to those political puzzles. Even the constitutions made after the coups could not attend to the interests of the masses.The leaders of the coups made the constitutions, which were to ensure that their evil interests were fulfilled. Such
constitutions appeared in Uganda, Sudan, Angola, Congo, Zimbabwe, Gabon, Togo and Rwanda”.

Hali hii ya viongozi kadhaa wa kiafrika ambao awali walionekana kuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi lakini polepole wakazivunja miguu katika za nchi zao ili waendelee kutawala hivyo kugeuka ving’ang’anizini sababu nyingine itakayopelekea mapinduzi kwa nchi hizo. Iwe ni mapinduzi ya umma ama vinginevyo lakini marais ng’ang’anizi kama Yoweri Museveni wa Uganda na mwenzake Paul Kagame wa Rwanda wamekalia kuti kavu kwani wananchi hawataki ufalme ama usultani bali wanataka demokrasia inayozingatia ukomo wa madaraka. Ikiwa watawala wa mataifa haya wataendelea kukaa madarakani basi joto kisiasa halitawaacha salama, wimbi la mabadiliko litawafagia mmoja baada ya mwingine kuelekea 2030.

Nova Kambota, 0712 544237
Alhamisi, 13 Novemba,2014
Dar es salaam, Tanzania


Nova Kambota ni mchambuzi na mwandishi wa siasa, hii ni sehemu ya maoni yake ya hivi karibuni kuhusu mapinduzi ya umma na mwelekeo wa siasa katika mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara. Nova Kambota anapatikana jijini Dar es salaam, simu +255712 544237, barua pepe; novakambota@gmail.com , Blog; http://novakambota.wordpress.com

0 TOA MAONI YAKO HAPA.:

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!