Audrey Mbugua akiwa nje ya mahakama ya awali.
MAHAKAMA Kuu imeamuru Baraza la Kitaifa
la Mitihani Kenya (KNEC), libadilishe jina cheti cha mlalamikaji ambaye
amekuwa akipigana atambuliwe kuwa mwanamke.
Jaji Weldon Korir jana Jumanne aliagiza
KNEC impe cheti kipya Bi Audrey Mbugua kikiwa na jina jipya
lililochapishwa katika gazeti rasmi la serikali.
Mlalamikaji, ambaye awali alitambuliwa kwa jina Andrew Ithubu Mbugua, alibadilisha jina lake kuwa Audrey Mbugua.
Bi Mbugua aliishtaki KNEC kwa kukataa
kubadilisha jina lake na kuondoa neno “mwanaume” katika cheti chake
kuonyesha kuwa ni “mwanamke” hata baada ya kuonyesha gazeti rasmi la
serikali lililochapisha mabadiliko kwenye jina lake.
Jaji Korir ameipa KNEC siku 45 kutayarisha cheti kipya na kumpa Bi Mbugua kikiwa na jina lake jipya.
Jaji aliamuru herufi “M” ambayo
inamaanisha “mwanaume” iondolewe katika cheti nambari 1855399 ambacho Bi
Mbugua alipewa na KNEC kwa jina la Ithubu Andrew Mbugua.
Jaji aliamuru cheti hicho kitolewe upya
kwa jina jipya la “Audrey Mbugua” bila herufi “M” (mwanaume) ama “F”
(mwanamke) akisema herufi hizo haziongezi maana au thamani yoyote kwa
cheti hata zikitolewa.
“Mlalamikaji ni mwanamke ambaye
amegubikwa kwenye mwili wa mwanamume ... maumbile ya kike ndani yake
yanazidi yale ya kiume na sina budi kuamuru mlalamikaji ajihisi
mkamilifu,” alisema Jaji Korir.
Jaji alisema katiba inaelezea wazi
kwamba “kila mtu anatakiwa kuchukuliwa kwa heshima na lazima kipengee
hiki kimfaidi mlalamishi kabisa.
Kutokitekeleza kwa manufaa yake ni kukiuka haki zake.”
Alisema kama Audrey atajihisi “mzima” ni
lazima akubalike jinsi alivyo na kumnyima haki ya kubadilisha jina lake
ni kukiuka haki zake na uhuru aliopewa na katiba.
Wakili wa Audrey, Bw Colbert Ojiambo,
aliIambia mahakama kuwa mlalamikaji alizaliwa jinsia yake ikiwa na utata
na amekuwa akitibiwa katika hospitali moja Nairobi.
Jaji Korir alisema ameangalia kesi nyingine za aina hiyo na kufikia uamuzi kwamba zote zinaegemea haki na heshima kwa binadamu.
“Mlalamikaji aliwasilisha mahakamani
gazeti rasmi la serikali lililochapishwa Januari 19, 2012 ambapo jina
lake limebadilishwa kuwa Audrey na Mkuu wa Sheria akasema hapingi
kubadilishwa kwa jina lake,” akasema jaji.
Alisema sheria nambari 9(1) ya mitihani
inasema cheti kinachotolewa na KNEC kinafaa kuonyesha jina la
mwanafunzi, nambari ya usajili na masomo aliyofanya, alama alizopata na
kwamba kinatolewa kwa utaratibu fulani.
Jaji Korir alisema sheria inaruhusu
mabadiliko kufanyiwa cheti na kwamba herufi ya kuonyesha jinsia haina
maana wala si lazima iwepo.
posted by paparazi
0 TOA MAONI YAKO HAPA.:
Post a Comment